1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Laschet kujiuzulu uwaziri kiongozi wa jimbo

25 Oktoba 2021

Armin Laschet, kiongozi wa chama cha kisiasa nchini Ujerumani, cha Christian Democratic CDU, atajiuzulu rasmi Jumattau kama waziri kiongozi wa jimbo la NorthRhine Westphalia.

https://p.dw.com/p/429hB
Düsseldorf | Laschet legt Amt als Ministerpräsident nieder
Picha: Bernd Schälte/Landtag NRW/dpa/puicture alliance

Laschet ambaye alikuwa wakati mmoja katika nafasi ya mbele ya kuelekea kumrithi mhafidhina mwenzake, Angela Merkel katika nafasi ya Ukansela alijikuta kuwa mtu aliyekisimamia chama chake wakati kikipata matokeo mabaya kabisa Septemba 26 ambayo hayajawahi kuonekana katika historia ya chama hicho katika chaguzi za bunge za shirikisho.

Armin Laschet ambaye ana umri wa miaka 60 alitangaza kwamba atajiuzulu uwaziri kiongozi wa NRW kabla hata ya uchaguzi wa bunge, hata pale ambapo atashindwa kuwa Kansela. Na leo Jumatatu ndio siku anayotimiza rasmi ahadi hiyo ya kujiuzulu. Hata hivyo atabaki kukaimu nafasi hiyo hadi pale atakapochukua nafasi ya kuwa mbunge katika bunge lijalo nchini Ujerumani, Bundestag siku ya Jumanne ambapo  litaapishwa rasmi.

Na siku ya Jumatano waziri wa uchukuzi wa jimbo hilo la NRW Hendrik Wuest anatarajiwa kuchaguliwa kuwa waziri kiongozi mpya katika kikao maalum cha bunge la jimbo hilo.  Wuest mwenye umri wa miaka 46 alichaguliwa kuiongoza CDU katika jimbo hilo mnamo siku ya Jumamosi.

Itakumbukwa kwamba wakati Laschet akiwa kiongozi wa chama cha CDU nchini Ujerumani, chama hicho na washirika wake kutoka jimbo la Bavaria Christian Social Union CSU walipata matokeo mabaya sana katika uchaguzi wa bunge uliopita, matokeo ambayo kwa hakika hayajawahi kuonekana katika historia ya vyama hivyo.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW