1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC ipo katika dharura ya kiafya

21 Agosti 2024

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakabiliwa na dharura kubwa ya kiafya, ikiwa na zaidi ya asilimia 96 ya visa vya Mpox vilivyoripotiwa duniani mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4jjTD
Waziri wa Afya wa DRC Samuel Roger Kamba
Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Samuel Roger Kamba.Picha: John Kanyunyu /DW

Wakati virusi vinaenea kwa kasi katika kambi za wakimbizi zilizofurika karibu na Goma, tatizo jingine lenye wasiwasi mkubwa linajitokeza ni kosefu wa udhibiti wa kiafya mipakani. Katika barabara kuu kati ya DRC na Rwanda, madereva wa malori na wasafiri wanaendelea kuvuka bila hatua zozote za kuzuia, na hivyo kuongeza hatari ya kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo.

Ukosefu huu wa uangalizi unawaweka mamilioni ya watu hatarini. Licha ya uzito wa hali hiyo, hakuna hatua madhubuti za kuzuia zilizowekwa mipakani na usafiri wa magari unaendelea kama kawaida. Barabara kuu kati ya DRC na Rwanda, ambayo ni lango muhimu kwa watu wanaotoka nchi za Afrika Mashariki, inabaki kuwa sehemu ya kuvuka bila udhibiti wa kiafya.

Hofu ya madereva wa Tanzania, Kenya na Uganda

Peru Lima | Wagonjwa wa Mpox | Hospitali ya Arzobispo Loayza
Daktari akimkagua mgonjwa aliye na vidonda vilivyosababishwa na maambukizi ya Mpox katika eneo la pekee kwa wagonjwa katika hospitali ya Arzobispo Loayza, huko Lima Agosti 16, 2022.Picha: ERNESTO BENAVIDES/AFP/Getty Images

Madereva wa malori kutoka nchi kama Tanzania, Kenya, na Uganda, hata hawajaambiwa kuhusu uwepo wa Mpox nchini Kongo. Aman Lukondo mmoja kati ya madereva hao anasema "Ninakuhakikishia kuwa hakuna mtu aliyenielezwa hadi sasa. Nimetoka Uganda kupitia barabara ya Chanika hadi Gisenyi, sijaona mtu akiniambia nijilinde, au kufanya hiki au kile. Nimevuka kama kawaida."

Nae James Wainaina amesema "Sikuambiwa habari ya huo ugonjwa. Hata hapa si niko Kongo saa hii? Hawajanieleza hiyo maneno. Isipokuwa wewe umekuja kuniambia. Na hata ukitembelea hawa madereva watakuambia kama kuna mtu ameambiwa. Na pia wangekuwa wanatueleza kwamba ugonjwa huu unahitaji hivi na hivi. Kama ningekuwa ninajua ningejibu."

Hali inaweza kuwa kama kipindi cha Janga la COVID-19?

Dereva wa Kenya, James Wainaina, anayesafiri mara kwa mara kwenye barabara zinazounganisha nchi za Afrika Mashariki na DRC, anaeleza wasiwasi wake unaozidi kuongezeka kuhusu mlipuko wa Mpox. Kwa maoni yake, ugonjwa huu wa virusi unaweza kuathiri vibaya kazi yao ya madereva wa mipakani, kama ilivyokuwa wakati wa janga la COVID-19.

Wainaina pia anaangazia athari za kisaikolojia kwa familia za madereva, "Inaweza kuathiri kwa sababu wakati wa corona tulitaabika sana. Kwa hivyo, hata wakati huu, kama hatua hazitachukuliwa kama wakati wa corona, utaathiri. Sasa si unaona katika hiyo maisha magumu. Unahitaji chakula, kikiisha huwezi kununua. Sisi ni watu tuna familia. Familia ikisikia baba ameshikwa Kongo na mgonjwa, nyumbani hawatakuwa na amani."

Wakati DRC inakabiliana na janga kubwa la kiafya, ukosefu wa hatua za udhibiti mipakani na uhamasishaji mdogo katika kambi za wakimbizi unaweza kuzidisha hali hiyo. DRC iko tayari kuishinda Mpox? Swali hili bado halijajibiwa, huku virusi vikiendelea kuenea. Mkoa wa Équateur ndio ulioathirika zaidi ukiwa tayari umerikodi visa 10,000, ukifuatiwa na Kivu Kusini, yenye visa 4,000 vya Mpox.

Soma zaidi:Ugonjwa wa Mpox sio janga kama COVID-19

Kwa mujibu wa wizara ya afia DRC, nchi ya kongo inahitaji kiwango cha chanjo milioni 3,4 kwa sasa.

DW, Goma.