Rwagasore alikuwa ni rafiki mkubwa wa Patrice Lumumba na Julius Nyerere. Waziri mkuu huyo wa muda mfupi wa Burundi, anaangaliwa kama shujaa anaekubaliwa na kila mtu katika nchi inayokabwa kila wakati na misuko suko.
"Burundi ya amani, yenye furaha na neema" ndio iliyokuwa ndoto ya Mwanamfalme Louis Rwagasore, aliyekuwa akivutiwa mno na masuala ya kiuchumi na kuamini fika kwamba uhuru unaweza kupatikana kwa njia ya amani.
"Eti damu yake, kama mwanamfalme ndio chanzo cha umashuhuri wake?
Ni hakika kwamba Louis Rwagasore amekulia katika nafuu za mwanamfalme: Alikuwa mtoto wa mwanzo wa Mwami Mwambutsa Bangicirenge, mfalme wa Burundi na kupatiwa elimu madhubuti katika mojawapo ya shule za sekondari zenye sifa kubwa nchini Rwanda, chini ya himaya ya Ubeligiji, Rwanda-Urundi ilikuwa wakati ule nchi moja tu. Baada ya kusomea taaluma kuhusu fani ya tawala na kilimo mjini Brussels ambako alijiunga na makundi ya wanaopigania uhuru na kukutana na wanafunzi wa kiafrika waliotokea kila pembe ya bara hilo, Rwagasore alirejea nyumbani mwaka 1956 na kugeuka mwanasiasa asiyejali machofu- haiba yake na ubora wa mikakati yake ikampatia umashuhuri.
Amefanikiwa vipi kuwaunganisha warundi ?
Louis Rwagasore alikuwa mwanadiplomasia stadi na mtu mwenye kipaji cha kuwaleta watu pamoja. Aliwavutia warundi kutokana na moyo wake wa ubunifu, kwanza alipoanzisha mashirika ya wakulima yaliyolengwa kuwapatia warundi wake kwa waume uwezo wa kudhdibiti shughuli zao za kilimo na kuachana na mtindo wa kulima kahawa tu. Kutokana na uhusiano aliokuwa nao pamoja na wanaharakati mashuhuri wapigania uhuru wa Afrika-Mwanamfalme Rwagasore akakutana mara kadhaa na Patrice Lumumba wa Kongo, alikuwa na mawasiliano pamoja na Gamal Abdel Nasser wa Misri na kuujenga mradi wake wa kisiasa pamoja na rafiki yake Julius Nyerere. Mradi wa mashirika ya wakulima haujafika mbali, lakini umempatia umashuhuri na akaunda chama chake; Chama cha Umoja na Maendeleo-UPRONA, tangu mwaka 1958, kilichokuwa na wanaharakati kutoka jamii mbali mbali.
Nafasi yake katika jukwaa la mashujaa waliopigania uhuru wa Afrika ni ipi?
Nchini Burundi, amegeuka kuwa shujaa anaesherehekewa katika sherehe zote za uhuru, anasalia kuwa kitambulisho cha mpito wa amani kuelekea uhuru na Burundi iliyoungana. Viwanja vya michezo, shule, maabara, njia-hishma kwa shujaa huyo wa taifa zimeenea kila mahala. Mwishoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Burundi, waliotia saini makubaliano ya Arusha ya mwaka 2000 hawachoki kusifu "uongozi wake wa kuvutia, mtu aliyeiepushia Burundi balaa la kutumbukia katika mapambano ya kisiasa kwa misingi ya kikabila". Kifo chake cha mapema kimemzuwia kuyashughulikia matatizo halisi ya taifa: matatizo ya kiuchumi hasa, matatizo ya ardhi na maendeleo ya jamii, matatizo ya elimu na matatizo mengi mengine ambayo tunajaribu kuyapatia ufumbuzi wetu wenyewe" kama alivyowahi kusema katika hotuba yake baada ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu.
Tamara Wackernagel, Antediteste Niragira na Gwendolin Hilse wamechangia kuandika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.
Mwandishi: Wackernagel,Tamara
Tafsiri: Kabogo, Grace Patricia
Mhariri: Mohammed Khelef