Kusini mwa Afrika kwaathirika zaidi na janga la corona
29 Januari 2021Eneo la Kusini mwa Afrika lilipongeza habari zilitolewa siku ya Alhamisi kwamba Umoja wa Afrika umepata dozi za ziada za milioni 400 za chanjo za virusi vya corona kwa nchi wanachama wake. Afrika Kusini inatarajia kupokea dozi yake ya kwanza ya chanjo ya AstraZeneca siku ya Jumatatu baada ya kuiidhinisha kwa matumizi ya dharura. Walakini, bado kuna sababu ndogo ya kusherehekea kwani mifumo ya huduma za afya ya eneo hilo imeanza kuelemewa kutokana na wimbi la pili la mripuko wa virusi vya corona. Athari za janga hilo zinajitokeza tofauti katika nchi hizi tano za kusini mwa Afrika.
Afrika Kusini: Yashutumu habari za uongo kuhusu chanjo
Serikali ya Afrika Kusini inasema inatarajia shehena ya kwanza ya dozi milioni moja ya chanjo ya AstraZeneca kutoka Taasisi ya Serum ya India mnamo Februari 1. Ni habari njema kwa nchi hiyo, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya visa vya maambukizi na vifo vilivyorekodiwa rasmi vya ugonjwa wa COVID-19 barani Afrika na ambayo pia inakabiliana na aina mpya ya maambukizi ya virusi hivyo.
Wafanyakazi wa huduma za afya wanatarajiwa kupewa kipaumbele
Waziri wa afya Zweli Mkhize amesema kuwa bado wako katika mpangilio kwa sababu suala hilo lilikuwa linailenga Januari na hakuna sababu yoyote ya kuwa na wasiwasi juu ya mabadiliko hayo.
Lakini kuongezeka kwa hadithi za uwongo kuhusu chanjo inayotarajiwa ya COVID-19 inazidi kuwa changamoto kwa viongozi. Nadharia moja maarufu inadai kwamba chanjo zitatumika kufuatilia watu kupitia mtandao wa simu ya mkononi wa 5G.
Habari hizi za uongo, ambazo kimsingi zinaenezwa kupitia mitandao ya kijamii, zinaonekana kupata wafuasi zaidi kila siku. Mkazi wa Afrika Kusini Davie Mashudu anasema haamini tena chanjo hiyo ni salama. Ameiambia DW kwamba hadhani chanjo hiyo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 inapaswa kufanywa lazima na kwamba yeye hataikubali.
Wakati huo huo, Rais Cyril Ramaphosa amewataka maafisa wa serikali kufanya kila wawezalo kufutilia mbali hadithi hizo za uwongo na njama kabla ya chanjo hiyo kutolewa kote nchini.
Afria Kusini inalenga kutoa chanjo kwa asilimia 67 ya raia wake ama takriban watu milioni 40 kufikia mwishoni mwa mwaka 2021.
Zimbabwe: Wachimba makaburi wana kazi nyingi
Hadi kufikia mwezi Desemba mwaka 2020, Zimbabwe iliweza kudhibiti visa rasmi vya maambukizi na kuwa na idadi ndogo.
Walakini, katika muda wa wiki tatu zilizopita vifo vinavyohusiana na virusi vya corona vimeongezeka kufikia takriban 50 kwa siku. Mawaziri wanne na wanasiasa kadhaa wa ngazi ya juu wamekufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 na kusababisha kuimarishwa kwa sheria za kudhibiti kuenea kwa maambukizi.
Zimbabwe sasa imerekodi rasmi visa 31,320 vya ugonjwa wa COVID-19 na zaidi ya vifo 1,000. Baada ya kufariki kwa mawaziri hao wanne kutokana na virusi hivyo, Rais Emmerson Mnangagwa aliahidi haraka kutolewa kwa chanjo kote nchini humo.
Zambia: Watu wengi waliokata tamaa wanajitibu wenyewe
Hospitali ya chuo kikuu cha Ualimu nchini Zambia (UTH) ambayo ndio kubwa zaidi ya rufaa nchini humo, inawatibu mamia ya wagonjwa kila siku. Lakini kulingana na Chitalu Chilufya, daktari na waziri wa zamani wa afya, idadi ya watu wanaofariki wanapokfikishwa hospitalini katika miezi ya hivi karibuni huenda ikahusishwa na ongezeko la watu kujitibu wenyewe dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.
Amesema raia wengi wa Zambia wanakunywa dawa za kutibu magonjwa mengine ama kutumia dawa tofauti za mitishamba. Maafisa wa afya wametoa wito kwa wananchi kutafuta huduma za mapema za matibabu iwapo watapata dalili zozote za ugonjwa huo.
Raia wa Malawai wakimbilia ufadhili wa vifaa vya kinga
Katika hospitali kuu ya Kamuzu mjini Lilongwe, vifaa vya kinga binafsi pamoja na gesi ya oksigeni zina uhaba. Hii ni hali ya kawaida katika hospitali nyingi nchini Malawi.
Huku vifaa vinavyotolewa na serikali vikiwa haba, watu waliojitolea kama Onjezani Kenani, raia wa Malawi anayeishi Uingereza, wameanza kupanga hafla za kuchangisha pesa kupitia mtandaoni ili kuzisaidia hospitali kuwa na vifaa vinavyohitajika kwa dharura.
Hata hivyo, waziri wa haki Titus Mvalo, ametoa wito kwa watu binafsi wanaochangisha pesa za kusaidia kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 kushirikiana kwa karibu na serikali kuzuia ulaghai.
Zaidi ya raia 550 wa Malawi wanaowajumuisha mawaziri wawili wamefariki kutokana na matatizo yanayohusiana na virusi vya corona.
Rais wa Tanzania anaendelea kukaidi na kukataa kuwepo kwa ugonjwa wa COVID-19
Kinyume na wenzake wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Rais wa Tanzania John Magufuli ameendelea kukaidi makubaliano ya matibabu ya ulimwengu kuhusu janga la COVID-19.
Siku ya Jumatano, alidai bila kutoa ushahidi kwamba chanjo zinaweza kuwa sehemu ya njama ya kigeni kueneza magonjwa na kuiba utajiri wa Afrika. Magufuli pia ameitaja chanjo ya COVID-19 kuwa hatari na isiyo ya lazima, badala yake akawasihi watu wamtumainie Mungu na wategemee tiba mbadala kama vile kujifukiza. Magufuli aliendelea kusema kuwa nchini Tanzania wameweza kuishi mwaka mmoja bila ya virusi vya corona na kwamba hata sasa hakuna mtu anayevaa barakoa huku akisema Mungu ni mkuu kuliko shetani na shetani atashindwa siku zote kwa kutumia magonjwa tofauti.
Serikali yake haijachapisha takwimu zozote za corona tangu katikati ya mwaka 2020 hali inayoweka idadi kamili ya sasa ya maambukizi yaliothibitishwa kuwa 509 na vifo 21. Shirika la Afya Duniani, (WHO) limeihimiza Tanzania kuzingatia sayansi huku mkurugenzi wa shirika hilo katika eneo la Afrika, Matshidiso Moeti, akituma ujumbe kwa mamlaka nchini Tanzania kupitia mtandao wa Twitter.