Kura zaendelea kuhesabiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati
28 Desemba 2020Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati haijatoa taarifa yoyote kuhusu idadi ya walioshiriki kwenye uchaguzi huo. Inakadikiriwa ni sehemu ndogo pekee ya raia wa nchi hiyo ndiyo walijitokeza kupiga kura kwa kuwa theluthi mbili ya eneo la Jamhuri ya Afrika ya Kati liko chini ya udhibiti wa makundi ya wapiganaji kwa miaka minane iliyopita. Lakini hakukutokea ghasia siku ya Jumapili, licha ya vitisho vya makundi ya waasi vya kuuteka mji mkuu, Bangui.
Msemaji wa serikali Ange Maxime Kazagui, alipongeza zoezi la upigaji kura, ambalo alisema ni juhudi za raia za kutaka kuweko na utawala wa haki. Baada ya kufungwa kwa vituo vya uchaguzi, Tume Huru ya Uchaguzi ilitangaza kwamba kulikuweko na changamoto chache za kiusalama kwenye baadhi ya vituo.
Mji mkuu Bangui ulibaki kuwa tulivu. Wanajeshi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, wanajeshi wa Afrika ya Kati na wanajeshi kutoka Rwanda walionekana kwa wingi wakipiga doria.
Kosoro za uchaguzi za zaripotiwa
Duru za Umoja wa Mataifa zinaelezea kwamba kulikuweko na machafuko ya hapa na pale nje ya mji mkuu Bangui ambako maelfu ya wapiga kura walizuiliwa kujitokeza kupiga kura.
Mjini Koui, kilomita 500 kaskazini magharibi ya mji mkuu Bangui, waasi walichukuwa vifaa vyote vya uchaguzi na kutishia kuwauwa wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi.
Kamati ya usalama wa uchaguzi ambayo iliundwa na serikali ilitangaza kwamba mikoa 12 kote nchini hazikuruhusiwa kupiga kura na waasi. Mji wa Bangui una wakaazi milioni moja miongoni mwa wakaazi milioni 4.9 kote nchini.
Uchaguzi huo tayari umezusha suala ya uhalali wa madaraka wa rais na wabunge 140 wanaotarajiwa kuchaguliwa.
Urusi ambayo inamuunga mkono Rais Faustin Archange Touadera toka mwaka 2018, ilipeleka wanajeshi 300 wa kuwapa mafunzo wanajeshi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Rwanda pia iliwapeleka wanajeshi wake kando na wale walioko kwenye kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa cha MUNISCA.
Zoezi la kuhesabu kura laendelea pia nchini Niger
Uchaguzi mwingine ni ule wa Niger ambako wagombea 29, wanawania kiti cha urais baada ya Rais Mahamadou Issoufou kumaliza mihula yake miwili.
Zoezi la kuhesabu kura linaendelea kote nchini na matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa baada ya siku kadhaa kutoka sasa. Wapigakura milioni 7.4 walitarajiwa kushiriki miongoni mwa wakaazi milioni 23. Tume ya Uchaguzi ilielezea kwamba hapakuripotiwa tukio lolote kubwa lililoathiri zoezi la upigaji kura.
Mohamed Bazoum, waziri wa mambo ya ndani mwenye umri wa miaka 60, anawania kwa tiketi ya chama tawala. Marais wawili wa zamani, mawaziri wakuu wawili wa zamani na mawaziri saba wa zamani ni miongoni mwa wagombea kwenye uchaguzi huo.
Mojawapo ya changamoto kubwa kwa rais mpya itakuwa ni usalama wa taifa hilo linalokumbwa na mashambulizi ya makundi ya kigaidi ambayo toka mwaka 2010 yalisababisha watu 500,000 kukimbilia nchi jirani na wengine kuwa wakimbizi wa ndani.