1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

'Kura ya maoni' ya Urusi yatwaa majimbo manne ya Ukraine

28 Septemba 2022

Moscow inasema kile inachokiita 'kura ya maoni' kwenye majimbo ya Ukraine inayoyakalia kimemalizika kwa zaidi ya 90% ya wapigakura kuamua majimbo hayo kujiunga na Urusi, huku jumuiya ya kimataifa ikilaani kura hiyo.

https://p.dw.com/p/4HR40
Ukraine Krieg, Scheinreferendum in Melitopol
Picha: RIA Novosti/Sputnik/SNA/IMAGO

"Kura ya maoni imefanyika. Tumekuwa tukiingojea kwa muda mrefu. Na sasa haya hapa matokeo ya kishindo. Itakuwa uongo tukisema hatukuyatarajia. Ninaamini juu ya Donbas, nawaamini watu wetu. Watu milioni 2, laki moja, elfu 16 na mia nane wamesema 'ndiyo' kujibu swali endapo wanaunga mkono Jamhuri ya Watu wa Donestk kujiunga na mamlaka ya Urusi. Tuliliota hili tangu mwaka 2014, sasa tumeweka historia. Tunaungana tena na nchi yetu kubwa ya asili, Urusi." Alisema Denis Pushilin, gavana wa mkoa wa Donestk, ambaye amewekwa na Urusi, akitangaza rasmi matokeo ya kile Urusi inachokiita 'kura ya maoni' usiku wa kuamkia Jumatano.

Kura hiyo ilipigwa kwenye mikoa ya Donetsk na Luhansk kwa upande wa mashariki na Kherson na Zaporizhzhia kwa upande wa kusini mwa Ukraine, ambapo kwa mujibu wa maafisa waliowekwa na Moscow, 99% ya wapigakura waliojitokeza katika jimbo la Donetsk, 98% wa jimbo Luhansk, 93% wa Zaporizhzhia na 87% katika jimbo la Kherson wametaka kujiunga na Urusi. 

Kwenye hotuba yake kwa taifa baada ya matokeo hayo kutangazwa, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alidai kuwa wakaazi wa majimbo hayo walilazimishwa kupiga kura chini ya mtutu wa bunduki na sasa watalazimishwa kupigana vita dhidi ya Ukraine, lakini ameapa kuilinda mipaka ya nchi yake.

Ukraine Kiew | Pressekonferenz: Wolodymyr Selenskyj
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine.Picha: Ruslan Kaniuka/Ukrinform/ABACA/picture alliance

"Tutawalinda watu wetu wa Kherson, Zaporizhzhia, Donbas, Kharkiv na Crimea. Kituko kilichofanywa kwenye maeneo hayo yanayokaliwa hakiwezi hata kuitwa igizo la kura ya maoani. Tulijuwa tangu mwanzo yapi yatakayokuwa matokeo yake. Hata shirika la ujasusi halikulazimika kufanya kazi kubwa. Takwimu zilizopikwa zimetangazwa. Urusi hata haijifichi. Jibu pekee kwa kitendo hiki cha mvamizi ni kuisaidia zaidi Ukraine na nawashukuru washirika wetu ambao wamethibitisha uungaji mkono wao kijeshi, kifedha na kwa vikwazo." Alisema Zelensky.

Jumuiya ya kimataifa yaja juu

Tayari Marekani kwa kushirikiana na Albania wameamuwa kuwasilisha azimio la kulaani kura hiyo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja huo, Linda Thomas-Greenfield, alisema kura hiyo inaweza kufunguwa njia kwa mambo mengine makubwa na mabaya zaidi, huku Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, akisema mataifa ya Magharibi kamwe hayataitambua kura hiyo. 

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amesema msimamo wa nchi yake kuelekea majimbo yanayokaliwa na Urusi nchini Ukraine haujabadilika, na kwamba haitambuwi unyakuzi unaofanywa na Urusi.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa NATO, Jens Stoltenberg, amesema kile alichokiita "kura ya maoni ya udanganyifu" haina uhalali na Canada imetangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi kutokana na kura hiyo.