Kura ya Baraza la Usalama kuhusu Gaza yaahirishwa tena
21 Desemba 2023Kura hiyo inayotaka usitishwaji wa muda wa mapigano kati ya Israel na Hamas imeahirishwa tena jana huku wanachama wa Baraza la Usalama wakibishana kuhusu maneno yaliyomo kwenye rasimu. Hayo ni wakati idadi ya vifo ikiendelea kuongezeka Gaza. Mjadala huo uliofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York umejiri wakati hali ikiendelea kuzorota Gaza.
Soma pia: Matumaini ya kusitishwa mapigano Gaza yaongezeka
Balozi wa Equador Jose Javier De La Gasca Lopez anayeshikilia urais wa kupokezana wa baraza hilo amesema wamekubaliana kuendelea na mazungumzo ili kuruhusu muda zaidi wa diplomasia. Amesema ofisi yake itapanga upya kura hiyo leo Alhamisi asubuhi saa za Marekani.
Wanachama wa baraza hilo wamekuwa wakilumbana kwa siku kadhaa kupata msimamo wa Pamoja kuhusu azimio hilo. Israel, ikiungwa mkono na mshirika wake Marekani, ambayo ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama aliye na kura ya turufu, inapinga matumizi ya neno "usitishwaji mapigano.”
Soma pia: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupigia kura azimio la Gaza
Macho yote sasa ni kwa Marekani
Chanzo cha kidiplomasia kimesema kuahirishwa kwa kura hiyo kumetokana na ombi la Marekani. Marekani inataka kubadilisha maandishi yanayosema kusitishwa kwa uhasama katika vita vya Israel na Hamas, na sehemu kuhusu kuupa Umoja wa Mataifa jukumu la ukaguzi wa malori ili kuhakikisha kuwa kweli yanasafirisha bidhaa za kiutu, mambo ambayo Israel inapinga.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jumatano kuwa hapatakuwa na usitishwaji mapigano Gaza hadi pale kundi la Hamas "litakapoangamizwa.” Kundi hilo limeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na baadhi ya mataifa ya Magharibi kama kundi la kigaidi.
Lakini Urusi na Jumuiya ya Kiarabu wameongeza shinikizo la kidiplomasia dhidi ya Israel ili kusitisha mapigano, wakitumia Jukwaa la Ushirikiano wa Urusi na nchi za Kiarabu nchini Morocco kuitisha usitishwaji mapigano.
Richard Gowan, mchambuzi katika shirika la kimataifa la kufuatilia migogoro, alisema kabla ya kuahirishwa tena kura hiyo kuwa "kila mmoja amekwama, akisubiria kuona kile Marekani itaama kukifanya.”
Kiongozi wa Hamas yuko Cairo
Wakati hao yakijiri, kiongozi mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh alielekea Cairo jana kwa mazungumzo kuhusu vita vya Gaza, ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa juhudi za kidiplomasia za kupatikana makubaliano mengine ya kusitisha mapigano na kubadilishana mateka na wafungwa wa Kipalestina katika wakati ambao mashambulizi ya Israel yanaendelea kupambana moto.
Ziara ya Haniyeh katika mji mkuu wa Misri imejiri siku moja baada ya Hamas kufyatua makombora ambayo yalisababisha ving'ora katikati ya Israel. Maafisa wa Afya katika Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na Hamas wamesema mpaka sasa Wapalestina 20,000 wameuawa, na zaidi ya milioni 1.9 wameyakimbia makaazi yao. Hiyo ni sawa na asilimia 85 ya jumla ya wakazi wa Gaza.
Pande zote zilianzisha hivi karibuni mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, yakisimamiwa na Misri, Qatar, na Marekani. Lengo ni kupatikana mpango mwingine wa kuweka chini silaha, na kuwaachia huru mateka zaidi ambao Hamas iliwachukua katika shambulizi lake la Oktoba 7, kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina wanaozuiliwa na Israel.
afp, reuters, ap, dpa