Kupanda miti kutapunguza mabadiliko ya tabia nchi; Utafiti
5 Julai 2019Mwanasayansi huyo anasema katika utafiti wake kuwa tunahitajika kupanda takriban miti trilioni moja, ama huenda zaidi.
Habari nzuri ni kwamba tunaweza kusaidia kuzuwia mabadiliko ya tabia nchi kwa kufanya kampeni kabambe ya kupanda miti, kwa mujibu wa utafiti mpya uliochapishwa jana Alhamis. Lakini kuna habari mbaya pia, kwa sababu tunahitajika kupanda miti katika eneo linalofikia ukubwa wa nchi kama Marekani ama nusu hivi ya bara la Afrika, na hata hivyo baadhi ya wanasayansi wanatia shaka juu ya hitimisho la utafiti wa waraka huo.
Juhudi kama hizo zitaweza kuhifadhi theluthi mbili ya gesi za kaboni zinazotolewa na binadamu na kupunguza viwango vya jumla katika anga hadi katika kiwango cha chini katika karibu karne moja, kwa mujibu wa utafiti ambao ulifanywa na ETH Zurich na kuchapishwa katika jarida la sayansi.
Utafiti huo ni wa kwanza kujaribu kuelezea ni miti mingapi dunia inaweza kusaidia dunia, wapi pa kupandwa miti hiyo na ni kiasi gani cha kaboni kinaweza kuhifadhiwa na miti hiyo.
Nafasi ya kupanda miti
Na kuna nafasi ya kutosha, anasema mtafiti huyo mwanasayansi kutoka Uswisi. Hata kwa kuwa na miji iliyopo hivi sasa na eneo la mashamba, kuna nafasi ya kutosha kupandwa miti mipya kuweza kuenea katika kilometa za mraba milioni 9. Eneo hilo ni takriban eneo sawa na Marekani.
Utafiti huo umepiga hesabu kwamba kwa muda wa miongo kadhaa, miti hiyo mipya inaweza kufyonza karibu tani za ujazo milioni 830 za gesi ya kaboni dioxide ambayo huhifadhi joto kutoka katika anga. Hii ni kiasi ya uchafuzi mkubwa wa kaboni kama ilivyotolewa na binadamu katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.
Manufaa makubwa yatakuja haraka kwasababu miti inaondoa kaboni zaidi kutoka katika hewa wakati ikiwa michanga, waandishi wa utafiti huo wanasema.
Uwezekano wa kuondoa kaboni nyingi zaidi uko katika maeneo ya tropiki.
Mataifa sita ambayo yana nafasi kubwa kwa kupanda miti mipya ni Urusi , Marekani, Canada, Australia , Brazil na China.