Kuondoka kwa Zuma, kutaleta mabadiliko Afrika Kusini?
17 Aprili 2017Maelfu ya raia wa Afrika Kusini wakiwa wanaandamani kumshinikiza Rais Jacob Zuma kuachia madaraka, inaleta picha kama vile Zuma ndiyo kikwazo pekee kinacholizuia taifa hilo kusonga mbele.
"Zuma lazima aanguke" umekuwa wito maarufu tokea kulipoanza maandamano dhidi ya rushwa na ukosefu wa ajira mwaka 2015. Hata wanachama wengi wa chama chake cha African National Congress (ANC) wamembandilikia Zuma.
Kumuondoa Zuma hata hivyo, huenda lisiwe suluhisho la matatizo yote yanayolikabili taifa hilo kwa mujibu wa wachambuzi.
Chama cha ANC kimejaa wanasiasa wenye mitazamo sawa na Zuma, na matatizo ya kiuchumi ya Afrika Kusini yameingiliana sana na ukosefu wa usawa uliorithiwa tokea wakati wa ubaguzi wa rangi, kiasi ya kwamba hata Zuma akiondolewa madarakani, huenda hatua hiyo isilete mabadiliko makubwa nchini humo.
Sifa ya Zuma imechafuka kutokana na msururu wa kashfa za rushwa, ikiwa ni pamoja na ile inayohusu utumiaji wa fedha za kodi ya umma kuifanyika marekebisho nyumba yake binafsi, na mafungamano ya karibu na familia ya kibiashara na yenye ushawishi mkubwa.
Wakati huo huo mamilioni ya Waafrika Kusini wanaishi makaazi yasiyo halali, na bila ya huduma za msingi, huku ukuaji wa uchumi ukiwa unazorota hadi kufikia asilimia 0.3 mwaka jana na zaidi ya robo ya idadi yote ya watu nchini humo imekosa ajira.
Matatizo ya kiuchumu ya Afrika Kusini yalizidi kuwa mabaya kufuatia uamuzi wa Zuma wa kumfukuza kazi waziri wa fedha anayeheshimika, Pravin Gordon.
Rushwa na utumiaji mbaya wa rasilimali
Wakati mkwamo wa kiuchumi kwa upande mmoja unatokana na sababu kama vile ukame na kuangua kwa bei za madini, lakini pia unatajwa kuwa unatokana na sera mbovu zenye makosa.
"Uharibifu na rushwa kwa pamoja, na uokoaji wa mfululizo wa makampuni ya serikali yasiyo na faida, yamepoteza kodi na rasilimali ambazo zingeweza kutumika katika kuendeleza sekta ya miundombinu." anasema Frans Cronje, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uhusiano wa Kikabila ya Afrika Kusini.
Tatizo si ukuaji wa polepole wa kiuchumi, lakini pia kukosekana kwa usawa kati ya matajiri na masikini walio wengi, anasema Nicolas Pons-Vignon, mtafiti wa uchumu katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand cha mnjini Johannesburg.
Afrika Kusini ni moja wapo ya nchi zilizo na viwango vya juu vya kukosekana kwa usawa katika dunia, kulingana na Benki ya Dunia.
Miongo miwili baada ya kumalizika kwa utawala wa kibaguzi, ukosefu wa usawa bado unaonekana kati ya watu weupe na weusi, licha ya kuibuka kwa tabaka la katikati la watu weusi.
Zaidi ya asilimi 70 ya mameneja wa kazi nchini humo ni watu weupe, licha ya kwamba watu weupe ni asilimi 8 huku watu wausi wakiwa ni asilimi 80 ya idadi nzima ya raia wa Afrika Kusini, kulingana na taasisi ya IRR.
Taasisi ya IRR inaongeza kuwa takriban watoto wote weupe wanahitimu shule ya sekondari ikilinganishwa na asilimi 67 ya watoto weusi.
ANC dhidi ya DA
Zuma sasa anajaribu kuwavutia watu weusi kwa kuwaahidi mabadiliko makubwa ya kiuchumi dhidi ya "uhodhi wa uchumi wa watu weupe."
Pons-Vignon anaziponda kauli za Zuma na kuzitaja kuwa ni porojo tupu, kutokana na kushindwa kwake kuitikia madai ya watu maskini pamoja na maandamano yao ya mfululizo, yaliyoendelea kwa miaka kadhaa, yanayodai shule bora na huduma bora ya afya bila ya kusogezwa mbele na vyombo vya habari.
Zuma anajali zaidi maslahi yake, kujitajirisha pamoja na kujilinda na kufunguliwa mashataka baada ya kumaliza muda wake madarakani, kwa mujibu wa wachambuzi.
Vuguvugu la ukombozi, lililomuweka madarakani Rais Nelson Mandela tokea kumalizika kwa ubaguzi nchini humo 1994, limeshuhudia kupoteza uungwaji mkono katika chaguzi za mitaa za 2016.
Hata hivyo, chama cha ANC bado kinategemewa kushinda uchaguzi mkuu wa 2019, ambao Zuma hatoweza kugombea baada ya kumaliza mihula yake miwili madarakani.
Lakini iwapo chama cha ANC kitashindwa na chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA), kinachoelemea upande wa biashara, basi serikali mpya itafanya kazi nzuri ya kuchochea ukuaji wa taifa, lakini haitokuwa na uwezekano mkubwa wa kuziba pengo kati ya watu matajiri na watu maskini, wanasema wachambuzi.
Serikali itakayoongozwa na DA, italeta mabadiliko ya kibiashara, jambo ambalo tayari limeshafanikishwa Afrika Kusini," anasema Pons-Vignon.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae
Mhariri: