1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la TPLF lawasilisha upya masharti ya mazungumzo

25 Oktoba 2022

Kundi la TPLF limewasilisha upya masharti ya kusitisha mapigano na ugavi wa msaada wa kibinadamu huku mazungumzo ya amani na serikali ya Ethiopia yanayoongozwa na Umoja wa Afrika yakianza Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/4IeDS
Äthiopien Debretsion Gebremichael, TPLF
Picha: REUTERS

Kituo cha televisheni cha Tigray kimeripoti kuwa baadhi ya masharti ya mazungumzo hayo ni kusitishwa kwa mapigano , kurejeshwa kwa huduma za kimsingi katika eneo la Tigray, kupelekwa kwa wakati kwa msaada wa kibinadamu kwa watu wa Tigray na kuondolewa kwa vikosi vya Eritrea kutoka eneo hilo. Kituo hicho pia kimethibitisha kuanza kwa mazungumzo hayo nchini Afrika Kusini ambapo ujumbe wa TPLF unaongozwa na afisa wa kamandi ya kijeshi Jenerali Tsadkan Gebretensae na msemaji wa kundi hilo Getachew Reda. 

Serikali ya Ethiopia yachukuwa udhibiti wa miji kadhaa 

Mazungumzo hayo yanajiri baada ya wanajeshi wa Ethiopia na washirika wao wanaojumuisha wanajeshi kutoka nchi jirani ya Eritrea, kuchukuwa udhibiti wa miji kadhaa mikubwa huko Tigray katika muda wa wiki moja iliyopita. Umoja wa Afrika ndio msimamizi wa mazungumzo hayo yanayoghubikwa na usiri. Duru za pande zote zimetoa taarifa za kukinzana kuhusu lini mazungumzo ya ana kwa ana yatakapoanza na Umoja huo wa Afrika pia umekataa kujibu maswali kutoka kwa vyombo vya habari.

Timu hiyo ya upatanishi ya Umoja wa Afrika katika mazungumzo hayo inatarajiwa kuwajumuisha  mjumbe wa Pembe ya Afrika Olusegun Obasanjo, aliyekuwa naibu rais wa Afrika Kusini Phumzile Mlambo-Ngcuka na aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Äthiopien | Premierminister Abiy Ahmed Ali
Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy AhmedPicha: Office of the Prime Minister Ethiopia/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Serikali inaonekana kuwa katika nafasi nzuri kuliko wapinzani wake wanapoingia katika mazungumzo hayo, ingawa serikali hiyo iko chini ya shinikizo ya mataifa ya kigeni yanayoijumuisha Marekani na Umoja wa Ulaya kusitisha mashambulizi yake.

Kiongozi wa TPLF asema adui aliyeingia Tigray 'atazikwa'

Siku ya Jumatatu ( 24.20.2022)  kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael alisema kuwa adui aliyeingia Tigray atazikwa, wakati kundi hilo likipoteza udhibiti wa miji muhimu kwa serikali ya nchi hiyo na vikosi vya washirika. Debretsion amekiambia kituo hicho cha televisheni cha Tigray kwamba watapata ushindi mkubwa kama ilivyofanyika mwaka 2021 na historia itathibitisha hilo.

Kiongozi huyo wa TPLF alikuwa anazungumzia mapigano ya mwaka 2021 ambapo vikosi vya uasi vilichukuwa udhibiti wa maeneo mengi ya Tigray ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa eneo hilo Mekelle kutoka kwa vikosi vya serikali ya Ethiopia.

Mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu, kupoteza makazi kwa mamilioni ya wengine na maelfu kukabiliwa na baa la njaa. Mzozo huo wa umwagaji damu umedhoofisha zaidi hali nchini humo na kutatiza mahusiano ya kidiplomasia na mataifa ya Magharibi.