Hamas lawaarifu Hezbollah juu ya usitishwaji mapigano
5 Julai 2024Vyanzo vimeeleza kwamba ujumbe wa Hamas ukiongozwa na naibu kiongozi wa kundi hilo Khalil Al Hayya, umemuarifu kiongozi wa Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah katika mkutano uliofanyika mjini Beirut kuhusu hatua mpya zilizopigwa juu ya suala la usitishaji vita.
Afisa mmoja mwandamizi wa Marekani jana alisema,kwamba kundi la Hamas limelegeza kwa kiasi kikubwa msimamo wake kuhusu uwezekano wa kufikia makubaliano na Israel juu ya suala la kuwaachilia mateka.
Kwa mujibu wa afisa huyo hatua hiyo inatowa matumaini ya kufikiwa makubaliano ya kupatikana usitishaji wa kudumu wa vita Ukanda wa Gaza.
Kadhalika kundi la Hamas limesema linapinga tamko lolote na misimamo inayounga mkono mipango ya kuingizwa vikosi vya kigeni katika Ukanda wa Gaza chini ya mamlaka yoyote.
Kundi hilo limesisitiza kwamba mamlaka ya Gaza ni suala linalowahusu Wapalestina tu na sio vinginevyo.