1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la Dola la Kiislamu laingia tena Kobane

Admin.WagnerD25 Juni 2015

Majihadi wa kundi la Dola la Kiislamu wameingia tena katika mji wa Kobane na wamekuwa katika mapigano makali na wapiganaji wa Kikurdi katikati ya mji huo wa Wakurdi ulioko nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1FnCu
Wanamgambo wa Kundi la Dola la Kiislamu.
Wanamgambo wa Kundi la Dola la Kiislamu.Picha: picture-alliance/Balkis Press

Wapiganaji wa kundi hilo la Dola la Kiislamu waliingia tena katika mji wa Kobane wakati wa alfajiri baada ya kuliripua gari lililotegwa mabomu karibu na kituo cha kivuko ambacho kinaunganisha mji wa Kobane na eneo la upande wa Wakurdi.

Mkuu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria lenye makao yake Uingereza Rami Abdel Rahman ameelezea mapigano yanayoendelea katikati ya mji wa Kobane kuwa ni makali sana.

Shirika la habari la Kikurdi Welati limesema wanamgambo wa Dola la Kiislamu walijipenyeza katika mji huo wa Wakurdi wakivalia sare za kijeshi za wapiganaji wa Kikurdi na wale wa Jeshi Huru la Syria.

Risasi zinafyatuliwa ovyo

Kwa mujibu wa shirika hilo wanamgambo hao wamekuwa wakifyetuwa risasi ovyo kwa yoyote yule anayetembea barabarani na kwamba mashambulizi yao yamepelekea maafa miongoni mwa raia.Serikali mjini Kobane imewasihi raia wasitoke nje ya nyumba zao hadi hapo watakapopata taarifa zaidi.

Mji wa Kobane.
Mji wa Kobane.Picha: picture-alliance/dpa/Antonio Pampliega

Wapiganaji wa Kikurdi wakisaidiwa na mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Marekani waliutwaa mji wa Kobane mwishoni mwa mwezi wa Januari baada ya wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu kuliteka eneo hilo.

Idriss Nassan afisa mwandamizi wa Wakurdi amesema wapiganaji wao wameidhibiti hali mjini Kobane na kwamba hivi sasa wanalitimuwa kundi la magaidi ambalo limeingia mjini humo na kusababisha machafuko na hofu miongoni mwa raia.

Wapiganaji wachache wa Kikurdi

Inaelezwa kwamba kulikuwa na wapiganaji wachache wa kikosi cha Wakurdi cha YPG katika mji huo kuweza kuzima shambulio hilo la ghafla kutokana na kwamba wengi wao wamepelekwa kwenye medani za mapambano karibu na mji wa Tel Abyad na kukiachia kituo cha polisi cha Asayesh kushughulikia usalama katika mjio huo.

Wapiganaji wa kikosi cha Wakurdi (YPG) mjini Kobane.
Wapiganaji wa kikosi cha Wakurdi (YPG) mjini Kobane.Picha: picture-alliance/dpa/S. Suna

Wanamgambo hao wa kundi la Dola la Kiislamu pia wameanzisha mashambulizi wakati wa usiku katika mji wa kaskazini mashariki wa Syria wa al-Hassakeh na kuviteka vitongoji viwili ambavyo vilikuwa chini ya udhibiti wa serikali ya Syria.

Takriban wanajeshi 30 tiifu wa serikali na majihadi 20 wameuwawa katika mapigano hayo ambayo bado yanaendelea.

Habari za hivi punde zinasema wapiganaji wa Dola la Kiislamu wamewauwa Wakurdi wa Syria 20 wakiwemo wanawake na watoto katika kijiji kilioko kusini mwa mji wa Kobane.

Uturuki imekanusha kwamba wapiganaji hao wameingia katika mji huo kwa kupitia kwenye ardhi yake na kusema kwamba habari hizo hazina msingi.

Mashambulizi ya kundi hilo la Dola la Kiislamu yanakuja baada ya majihadi hao kupata mfulululizo wa vipigo na kushindwa na Kikosi cha Wakurdi cha YPG ambapo wiki iliopita waliuteka mji muhimu wa Tel Abyad ulioko eneo la mpakani na Uturuki.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/AFP

Mhariri : Iddi Ssessanga