1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu za mauwaji ya halaiki ya Holocaust Magazetini

Oumilkheir Hamidou
28 Januari 2020

Kumbukumbu za mauwaji ya halaiki ya wayahudi, miaka 75 tangu kambi za maangamizi za Auschwitz zilipokombolewa, na vitisho dhidi ya wanasiasa mashinani ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/3WuPc
75 Jahre Befreiung von Auschwitz
Picha: Reuters/N. Savosnick

Tunaanzia Auschwitz nchini Poland ambako jana walimwengu walijionea na kusikia jinsi manusura wa kambi hizo za maangamizi  walivyokuwa wakisimulia yale waliyotendewa na wanazi miaka 75 baada ya kambi hizo kukombolewa. Gazeti la "Passauer Neue Presse" limewanukuu baadhi ya manusura waliosema:"Baadhi ya wakati kulikuwa na harufu ya nyama ya binaadam."Matamshi kama hayo yanamfanya mtu atambue moja kwa moja  ukatili uliokithiri uliotendeka wakati wa mauwaji ya halaiki ya wayahudi Holocaust, mamilioni ya watu waliokuwa hai, waliokuwa wakivuta pumzi, waliokuwa na joto lao la mwili, walivyoangamiziwa maisha na kudhalilishwa.

Ushahidi huo wa mateso na vifo, wanaoweza kuutoa ni manusura tu. Jana, kwa mara nyengine tena ulimwengu mzima uliwakodolea macho.Yote waliyoyasimulia kuhusu maovu ya Ausschwitz na ambayo yameonyeshwa na televisheni ni nyaraka zinazobidi kuhifadhiwa kwa vizazi vinavyokuja. Zaidi ya hayo nyaraka hizo za maovu ni hazina yenye thamani kubwa ambayo binaadam tunabidi tuitunze nyoyoni mwetu na kukumbuka daima, manusura watakapokuwa wameshaiaga dunia."

Wanasiasa mashinani mashakani

Mada nyengine inayogonga vichwa vya habari magazetini ni kuhusu vitisho dhidi ya wanasiasa wa serikali za mitaa. Hofu zimeenea miongoni mwa wanasiasa hao baada ya mkuu wa serikali ya Kassel, kaskazini mwa jimbo la Hesse kuuliwa. Gazeti la Mittelbayerische Zeitung" linaandika: "Idara ya upelelezi wa ndani BKA  imeorodhesha kadhia zaidi ya 1200 za visa vya kuhujumiwa maafisa wa serikali pamoja na wanasiasa wa mikoani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Miongoni mwao ikiwa ni pamoja na shambulio lililoangamiza maisha ya mkuu wa serikali ya Kassel, Walter Lübcke.Tatizo hili si jipya.

Yeyote mwenye kuwakilisha masilahi ya jamii na kupitisha maamuzi yanayoshawishi kwa njia moja au nyengine maisha ya wengine anageuka rafiki au adui wa kambi moja au nyengine. Historia inatukumbusha visa kadhaa vya matumizi ya nguvu dhidi ya wanasiasa-na kila shambulio ni la kulaaniwa. Ripoti kuhusu visa kama hivyo zinashtuwa. Na kuhuzunisha. Anaetaka kupambana na uhalifu huo anabidi adai hatua kali zichukuliwe, na sheria kali zipitishwe. Muhimu zaidi lakini ni kuwaunga mkono na kuwasifu wote wale ambao wanawajibika mitaani na mijini kila kukicha."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga