Kumbukumbu ya kimataifa ya mauaji ya Wayahudi ya Holocaust
27 Januari 2019"Wale ambao hawakumbuki yazamani wanaweza kuyarudia." Nukuu hiyo ya mwanafalsafa Mhispania - Mmarekani na mwandishi George Santayana inaweza kuonekana katika kambi ya mateso ya Auschwitz. Kukumbuka mauaji dhidi ya Wayahudi, Holocaust kimsingi imekuwa juhudi za taifa la Ujerumani kwa miaka mingi , kutoka kwa maafisa hadi wabunge. Mvuto kutoka kwa umma bado uko imara pia. Makambi ya zamani ya mateso pamoja na maeneo mengine ya kumbukumbu yanapata watu wengi wanaoyatembelea.
Na bado, mashirika ya Wayahudi yanasema yameshuhudia ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani. "Bingwa wa dunia wa kumbukumbu anapoteza vita dhidi ya chuki za hivi sasa dhidi ya Wayahudi," anasema Meron Mendel, mkurugenzi wa kituo cha elimu mjini Frankfurt cha Anne Frank. Wasi wasi huo unaungwa mkono na uchunguzi uliofanyika hivi karibuni na shirika la Umoja wa Ulaya kwa ajili ya haki za msingi katika mataifa 12 ya Ulaya. Uchunguzi huo umegundua kwamba katika mwaka uliopita, Wayahudi nchini Ujerumani hawakukabiliana tu na uhasama zaidi kuliko mwaka uliopita, lakini pia wamekabiliwa na uhasama huo kuliko katika nchi nyingine.
Kiasi ya asilimia 41 ya Wayahudi nchini Ujerumani wamesema walikuwa wahanga wa uhasama na chuki dhidi ya wayahudi, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 28 katika mataifa mengine yaliyofanyiwa uchunguzi.
Wasi wasi kwa Wayahudi
Kile kinachowatia wasiwasi zaidi Wayahudi nchini Ujerumani ni matamko yanayotolewa na wanasiasa kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany AfD. Mwaka jana, kiongozi wa chama hicho Alexander Gauland alisema kwamba " Hitler na Wanazi ni tone tu la kinyesi cha ndege katika zaidi ya miaka elfu ya mafanikio katika historia ya Ujerumani."
Na miaka miwili iliyopita kiongozi wa AfD wa jimbo la Thuringia Bjoern Hoecke alitoa wito wa "kubadilika kwa digrii 180" katika utamaduni wa Ujerumani, kwa kuangalia "hasira" ambazo Gauland na Hoecke walizosababisha. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas ametoa wito kwa mtazamo mpya katika kuwafundisha watu juu ya Holocaust.
"Kile tunachohitaji hivi sasa ni mtazamo mpya wa kuadhimisha matukio ya kihistoria kwa manufaa ya hivi sasa," Maas aliandika katika makala kama mwandishi mwalikwa katika gazeti la kihafidhina la Welt am Sonntag ikiingiliana na siku ya kimataifa ya kumbukumbu ya Holocaust leo Jumapili (27.01.2019).
Usiku wa vioo
Amesema kuwa kusonga mbele, historia inapaswa kuangaliwa sio tu kama suala la kukumbuka matukio yaliyopita lakini pia kama suala la kuyaelewa matukio hayo.
Mwanasiasa huyo kutoka chama cha SPD alikiri kwamba enzi za Wanazi na mauaji ya Holocaust yanatupwa kando kila muda unavyokwenda. "Kwa mtu aliyezaliwa leo, "Usiku wa vioo vilivyovunjika" mwaka 1938 ni muda mrefu sana kama utawala wa kansela Bismark mwaka 1971 nilipozaliwa. Hii inabadilisha jinsi matukio kama hayo yanavyokumbukwa.
Masinagogi na biashara zilizokuwa zinamilikiwa na Wayahudi nchini Ujerumani ziliporwa na kuchomwa moto Novemba 9, 1938, siku ambayo ilikuja kufahamika kama "usiku wa kuvunjika vioo."
Siku ya kimataifa ya Holocaust ni kumbukumbu ya kuuwawa Wayahudi wa Ulaya milioni 6 na wote waliouwawa katika kambi za mauaji za enzi za Wanazi. Vikosi vya jeshi la iliyokuwa Umoja wa Kisovieti vilikomboa kambi ya mateso ya Auschwitz Januari 27, 1945.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Bruce Amani