Kucheza dhidi ya Brazil ni ndoto ya wachezaji wa Ubelgiji
4 Julai 2018Brazil wanaonekana kupigiwa upatu kushinda pambano hili katika kile ambacho kocha wa Ubelgiji Roberto Martinez alichokieleza kuwa ni "ndoto" kwa wachezaji wake wakati mataifa hayo mawili yatakapokutana katika mchezo wa robo fainali mjini Kazan siku ya Ijumaa.
"Timu hizi mbili zimejengwa kufunga mabao na kushinda michezo. Dhidi ya Brazil, haitakuwa juu ya umiliki wa mpira, lakini kile unachoweza kufanya na mpira. Hicho ndio kila kitu katika kombe hili la dunia," Wahispania waliviambia vyombo vya habari vya Ubelgiji leo Jumatano(04.07.2018).
"Tunafahamu kile tunachokiweza lakini Brazil wako mbele, wakituweka katika nafasi tofauti kabisa," aliongeza Martinez.
"Lakini ni mchezo ambao kama tumo katika ndoto kwa wachezaji wetu, wamezaliwa kucheza katika mchezo kama huu. Kwa kawaida tunataka kushinda lakini hatutarajiwi kufanya hivyo na hii ndiyo tofauti muhimu."
Martinez alishuhudia kikosi chake kikiwa katika ukingo wa kuondolewa mashindanoni na kupata ushindi wa dakika za mwisho wa mabao 3-2 dhidi ya Japan katika duru ya timu 16 siku ya Jumatatu, na kukata tikiti ya kukutana na mabingwa mara tano wa kombe la dunia Brazil.
Katika baadhi ya nyakati mjini Rostov - on - Don, Ubelgiji ilionekana kukwazika na mbinu za mbinyo za Japan na walihitaji zaidi ya saa nzima kujitoa na kuweza kurejea katika mchezo kutoka nyuma baada ya kutandikwa mabao 2-0 na Japan.
Kwa mchezo wa Ijumaa mbinu huenda zitakuwa rahisi.
"Dhidi ya timu kama Brazil , ni lazima ushambulie na kulinda lango na wachezaji 11. Hatuzungumzii juu ya mfumo lakini kufahamu kile tunachopaswa kufanya wakati tuna mpira," kocha huxo alisema.
Sidhani iwapo utakuwa mchezo wenye siri nyingi. Tunapaswa kulinda kandri tunavyoweza na kisha kuwasababishia maumivu makali wakati tukiwa na mpira. Itakuwa rahisi hivyo na kikosi hiki kiko tayari kwa hilo."
Uingereza ilielekeza hisia zake katika mchezo mgumu wa robo fainali dhidi ya Sweden wakati wakilenga kuendeleza ushindi wake dhidi ya Colombia, katika ushindi wake wa kwanza kupitia mikwaju ya penalti katika kombe la dunia.
England haibweteki baada ya ushindi huo wakati ikijitayarisha kupambana na Sweden katika mchezo wa robo fainali siku ya Jumamosi.
"Ni wagumu sana kupambana nao," kocha Gareth Southgate alisema kuhusiana na kikosi cha Sweden. "Kwa wakati huu tuko juu kama tiara lakini nadhani ni lazima tushuke. Ni mchezo mkubwa kushiriki. "Nawaheshimu sana Sweden. rekodi yetu dhidi yao sio nzuri. Mara kadhaa tumewadharau."
Pambano la Jumamosi mjini Samara ni la tatu baina ya timu hizo katika kombe la dunia, kufuatia sare katika awamu ya makundi mwaka 2002 , bao (1-1) na 2006 bao (2-2). Pia walikutana mara mbili katika ubingwa wa bara la Ulaya , ambapo Sweden ilishinda kwa mabao 2-1 mwaka 1992 na Uingereza ikashinda kwa mabao 3-2 mwaka 2012.
Michezo mingi ya kirafiki baina ya timu hizo imekuwa ngumu kwa kila upande kwa hiyo mambo madogo madogo yanaweza kuleta mabadiliko, kama vile Sweden ilicheza mchezo wake wa kundi la 16 bora masaa manne kabla ya uingereza na ilihitaji dakika 90 tu kuwaondoa Uswisi kwa bao 1-0. Uingereza kwa upande wake ilihitaji dakika 120 , baada ya goli la dakika za mwisho la Colombia la kusawazisha baada ya bao la kuongoza la nahodha wa England, Harry Kane kwa mkwaju wa penalti.
Lakini usiku wa jana ulikuwa muhimu sana kwa kikosi hiki kichanga cha kocha Southgate , ambaye binafsi alikosa mkwaju wa penalti katika nusu fainali ya Euro 1996 dhidi ya Ujerumani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga