Korea Kusini yamwita balozi wa Urusi mjini Seoul
21 Juni 2024Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini imesema nchi hiyo "imeitaka Urusi kuacha mara moja ushirikiano wa kijeshi na Korea Kaskazini na kuheshimu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa". Kuitwa kwa balozi wa Urusi mjini SeoulGeorgy Zinoviev kunafanyika siku mbili baada ya Rais Putin kusaini makubaliano ya "kina ya ushirikiano wa kimkakati" yanayojumuisha ahadi ya kusaidiana iwapo nchi moja itashambuliwa.
Seoul imemweleza balozi wa Urusi iliyomuita kwamba nchi hiyo inapaswa kutekeleza wajibu wake kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kulingana na naibu waziri wa kwanza wa Korea Kusini Kim Hong-kyun, "ukiukaji wa maazimio ya Baraza la Usalama na kuiunga mkono Korea Kaskazini kunaweza kuathiri usalama na kuwa na athari kubwa katika uhusiano wa Korea Kusini na Urusi."
Korea Kaskazini imekuwa chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2006 kutokana na mpango wake wa nyuklia uliopigwa marufuku. Soma: Putin kusaini mikataba ya ushirikiano wakati wa ziara mjini Pyongyang
Hatua hizo ziliungwa mkono na Urusi hapo awali, lakini Putin alipozuru Pyongyang alisema kwamba vikwazo hivyo vinapaswa kupitiwa upya. Seoul, ambayo ni muuzaji mkubwa wa silaha, ilisema wiki hii kwamba "itafikiria upya" juu ya sera yake ya muda mrefu ambayo inazuia kusambaza silaha moja kwa moja kwa Ukraine, kufuatia makubaliano ya ulinzi ya Pyongyang na Moscow. Hata hivyo, Putin aliionya Korea Kusini kwamba kama itakuwa imefanya kosa kubwa ikiwa itaiapatia silaha Ukraine.
Soma pia: Korea Kaskazini kuacha kutuma maputo ya taka Korea Kaskazini
Kwingineko, jeshi la Korea Kusini limedai kufyatua risasi za onyo baada ya wanajeshi wa Korea Kaskazini kuvuka kwa muda mfupi mpaka ulio na ulinzi mkubwa ikiwa ni uvamizi wa tatu ndani ya mwezi huu. Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia imekuwa ikiimarisha eneo lake la mpaka katika miezi ya hivi karibuni, ikiongeza njia za kiufundi na kuweka mabomu zaidi ya ardhini, jambo ambalo limesababisha "maafa" kati ya wanajeshi wake kutokana na milipuko ya bahati mbaya, kulingana na Korea Kusini.
Huku hayo yakijiri, Makamu Kansela wa Ujerumani Robert Habeck ambaye yuko ziarani Korea Kusini, ameishukuru nchi hiyo kwa msimamo wake wa pamoja wa kuiunga mkono Ukraine katika mapambano yake dhidi ya uvamizi unaoendelea wa Urusi.
Habeck ambaye pia ni waziri wa fedha wa Ujerumani aliwasili Korea Kusini siku ya Jumatano katika ziara yake ya kwanza ya kidiplomasia katika taifa hilo la Asia Mashariki.
Mapema siku ya Ijumaa, kiongozi huyo aliutembelea mpaka wa Korea Kusini ulio na ngome kubwa unaopakana na Korea Kaskazini wakati mivutano katika rasi ya Korea ikizidi kuongezeka.