Korea Kaskazini yashtumiwa kwa kuwapeleka wanajeshi Urusi
24 Oktoba 2024Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Korea Kusini, Cho Tae-yong, amewaambia wabunge nchini humo kwamba wanajeshi 3,000 wa Korea Kaskazini walikuwa wakipewa mafunzo ya kutumia vifaa ikiwa ni pamoja na droni kabla ya kupelekwa katika uwanja wa vita nchini Ukraine.
Korea Kaskazini yakanusha kupeleka wanajeshi Urusi
Kwa upande wake, wakati wa ziara yake mjini Rome nchini Italia, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, aliwaambia waandishi wa habari kwamba wanao ushahidi kwamba kuna wanajeshi wa Korea Kaskazininchini Urusi.
Hata hivyo, wawili hao hawakutoa maelezo ya jinsi walivyogunduwa uwepo wa wanajeshi hao wa Korea Kaskazini nchini Urusi, huku maswali mengi yakiibuka kuhusu athari za ushiriki wa Korea Kaskazini kwenye vita nchini Ukraine.
Zelansky adai kuonekana kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini
Siku ya Jumatatu, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliwaambia waandishi wa habari kwamba maafisa wa kijeshi wa Korea Kaskazini wamekuwa wakionekana katika maeneo yaliyotekwa na Urusi ijapokuwa hakuthibitisha ni lini hasa.
Maafisa wa Ujerumani na Uingereza pia wameingilia suala hili huku Korea Kusini ikidokeza kwamba inaweza kuisaidia Ukraine na silaha za kijeshi iwapo itathibitishwa kuhusika kwa Korea Kaskazini.
Hata hivyo, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, amesema bado hawafahamu idadi kamili wala aina ya wanajeshi wanaokwenda nchini Urusi, ama mahala wanapopigana na dhidi ya nani.
Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, John Healey, amesema hakuna tu wasiwasi wa uwezekano wa kutanuka kwa mapigano hayo barani Ulaya, lakini pia kuna wasiwasi wa kiusalama katika eneo la India na Pasifiki.
Baraza la chini la bunge la Urusi waidhinisha mkataba wa ulinzi
Wabunge katika baraza la chini la bunge la Urusi wamepiga kura kwa kauli moja kuidhinisha mkataba wa ulinzi na Korea Kaskazini.
Mkataba huo ambao unatowa idhini ya nchi moja kuisaidia nyengine pale inapotishiwa kijeshi, sasa utapelekwa kwenye baraza la juu la bunge hilo kwa ajili ya kuidhinishwa.
Ikulu ya Kremlina yakataa kuzungumzia tuhuma dhidi ya nchi yake
Ikulu ya Kremlin imekataa kuzungumzia chochote kuhusu tuhuma za kuwapo wanajeshi wa Korea Kaskazini, lakini imesema kuwa mkataba wake na Korea Kaskazini una maana ya "wazi" na maneno yake ‘'hayahitaji kufafanuliwa".