Korea Kaskazini yashindwa tena kutuma satelaiti angani
24 Agosti 2023Roketi hiyo ilishindwa kuendelea na safari kutokana na kile maafisa wa Taasisi ya Maendeleo ya Teknolojia ya Anga za Mbali ya Korea Kaskazini wamesema ni hitilafu kwenye mfumo wake wa dharura.
Taasisi hiyo imesema, safari ya roketi hiyo ilikwenda vizuri katika hatua mbili za awali na hitilafu ya kiufundi ilitokea wakati wa hatua ya tatu.
Korea Kaskazini ilikuwa inajaribu kwa mara nyingine kupeleka satelaiti angani baada ya jaribio kama hilo kushindwa hapo Mei 31.
Satelaiti hiyo iliyopewa jina la Malligyong-1 ingeisaidia Pyongyang katika operesheni zake za kijeshi.
Hata hivyo jaribio hilo limekoselewa na mataifa jirani ikiwemo Japan na Korea Kusini huku Marekani ikisema linakiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa vinavyoizuia Korea Kaskazini kurusha vyombo vya masafa.