Kongo yaituhumu M23 na Rwanda kuhujumu usafiri wa anga
30 Julai 2024Imesema wanafanya hivyo kwa kuingilia mfumo wa mawasiliano unaotumia teknolojia ya GPS. Katika taarifa yake iliyotolewa usiku wa kuamkia leo, serikali ya Kongo imesema ilifanya uchunguzi kubaini chanzo cha hitilafu kwenye mfumo wa mawasiliano ya kuongoza ndege unaotumia teknolojia ya GPS baada ya ripoti za kuwepo mparaganyiko.
Taarifa hiyo imesema uchunguzi wake umegundua vikosi vya jeshi la Rwanda ndiyo vimehusika kusababisha hitilafu hiyo kwa kuhujumu mfumo uliopo. Imesema vikosi hivyo vimekuwa vikituma mawimbi tofauti ya mawasiliano ya GPS kwa dhamira ya kuvuruga ule uliopo.
Kongo imeonya kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa usafiri wa anga na kuziweka rehani juhudi za kiutu zinazotegemea usafiri huo kupeleka misaada kwa maelfu ya watu waliokimbia mapigano.