Kongamano la Davos na idadi ya wabunge Magazetini
22 Januari 2020Katika milima ya theluji ya Davos nchini Uswisi, viongozi wa kisiasa, kiuchumi na wa mashirika ya huduma za jamii wanahudhuria kongamano la 50 ambalo mwaka huu linagubikwa na suala la mabadiliko ya tabianchi. Mafahali wawili wamekutana linaandika gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" likimaanisha kwa upande mmoja rais wa Marekani Donald Trump na kwa upande wa pili mwanaharakati, msichana mdogo anaepigania usafi wa mazingira, Greta Thunberg.
Gazeti linaendelea kuandika:"Katika wakati ambapo rais wa Marekani Donald Trump anatoa hotuba kusifu nguvu za kiuchumi za Marekani, Greta Thunberg amelitumia jukwaa la Davos kuwaonya viongozi hao. Wafuasi wa vuguvugu la "Fridays for Future" wanadai kuwa na dunia iliyo salama zaidi..Lakini hawazingatii nguvu na uwezo wa demokrasia na mfumo wa soko huru.
Mustakbali haupo katika uchumi kijani wa mpangilio au mfumo ambapo wasomi watahubiri jinsi ya kuachana na baadhi ya vitu. Zaidi kuliko yote tunabidi tubuni mfumo wa neema kwa ulimwengu usiochafua mazingira na ambao hivi karibuni idadi ya wakaazi wake itafikia watu bilioni nane. Na hilo linawezekana.
Ujinga na hofu si dawa
Gazeti la "Hannoverssche Allgemeine linakosoa misimamo ya mafahali haoa wawili na kuandika:Trump na Thunberg wanafuata malengo tofauti. Wanapigania misimamo mikali. Kwa namna hiyo hakuna kati yao atakaetoa muongozo wa jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambao viongozi wanaohudhuria kongamano la kiuchumi la Davos watauona ni muhimu. Kuzidi hali ya ujoto duniani ni tatizo kubwa. Lakini pia ujinga na hangaiko si ufumbuzi."
Mageuzi ya kanuni za uchaguzi yatasalia kuwa ndoto
Mada ya pili magazetini inamulika mjadala unaohanikiza kuhusu mageuzi ya kanuni za kupiga kura kwa lengo la kupunguza idadi ya wabunge nchini Ujerumani. Gazeti la "Volksstimme" linaandika:"Yadhihirika kana kwamba mada hiyo inazungumzwa kila upande. Lakini kimsingi ni maneno matupu. Tangu sasa mtu anaweza kuashiria kwamba mageuzi ya kanuni za kupiga kura yanayotakiwa na bunge la shirikisho Bundestag yatashindwa.
Na kuna nafasi nzuri idadi ya wabunge ikazidi kuongezeka uchaguzi mkuu utakapoitishwa. Jibu kwanini hakuna kitakachobadilika ni rahisi: Vyama vingi havitaki mageuzi yatakayopelekea idadi ya viti kupunguzwa. Wabunge wana ofisi mbili kila mtu na wasaidizi kadhaa. Mageuzi ya kanuni za kupiga kura yatamaanisha kupungua idadi ya wabunge. Na hali hiyo inaweza kuzua hatari kwa wengi katika enzi hizi ambazo walinzi wa mazingira na AfD wanavuma. Na zaidi ya hayo hakuna anaejipiga kumbo mwenyewe, seuze tena kama marupurupu yatapungua.