1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kocha wa Uholanzi asema hawaiogopi Uhispania

10 Agosti 2023

Kocha wa Uholanzi Andries Jonker anasema "anajua kila kitu" kuihusu timu ya Uhispania kuelekea mechi yao ya robo fainali katika Kombe la Dunia la Wanawake hapo Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4V03n
FIFA Kandanda Wanawake Marekani vs Uholanzi
Wachezaji wa Uholanzi wakisherehekea goli dhidi ya marekaniPicha: Amanda Perobelli/REUTERS

Jonker anasema yote haya ni kwasababu ya mchezaji wake Damaris Egurrola ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa Uhispania.

Egurrola aliichezea Uhispania mechi moja katika mechi ya kirafiki na katika timu za wachezaji chipukizi aliicheza mara kwa mara ila kiungo huyo wa kati sasa anaichezea Uholanzi na huenda akaanizishwa katika mechi ya Ijumaa huko Wellington, New Zealand.

Jonker na makocha wake wa kiufundi wamefahamishwa pia kuhusiana na kile wanachostahili kukitarajia kutoka kwa beki Merel van Dongen anayeichezea Atletico Madrid huku Stefanie van der Gragt na Lieke Martens wote wakiwa waliichezea Barcelona.

"Tunaiheshimu Uhispania kwa mafanikio yake ya zamani, kwa jinsi wanavyocheza na jinsi wanavyonuia kucheza," alisema Jonker. "Lakini hatuwaogopi, tutacheza mechi yetu na ni juu yao kuamua jinsi watakavyokabiliana nasi."

Uholanzi walifika robo fainali kwa kuilaza Afrika Kusini 2-0 katika raundi ya 16 bora nao Uhispania walifika hatua hiyo ya nane bora kwa kuigaragaza Uswisi 5-1.

Mechi ya kufa na kupona

Kocha wa Uhispania Jorge Vilda amemtaja mshambuliaji wa Uholanzi Martens, aliyecheza katika fainali ya 2019 na ambaye anashiriki kombe lake la tatu la dunia, kama kitisho kikubwa wanachokiona katika timu hiyo ya Uholanzi.

Kandanda Wanawake Uhispania vs Costa Rica
Wachezaji wa Uhispania wakisherehekea bao dhidi ya Costa RicaPicha: Catherine Ivill/Getty Images

Uhispania haijafika umbali wa hatua ya robo fainali katika mashindanohayo ya kuwania ubingwa wa dunia kwa wanawake na beki wao Ivana Andres amekiri kwamba ana wasiwasi kiasi cha haja.

"Hizi ndizo mechi tunazopenda kucheza, mechi za kufa na kupona," alisema Andres. "Tutafanya kila kitu kwa kuwa tunataka kuweka historia."