1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar 2022: Senegal, England, USA na Uholanzi zasonga mbele

Daniel Gakuba
30 Novemba 2022

Senegal imekuwa timu ya kwanza ya Afrika kukata tiketi ya kuingia awamu ya kumi na sita bora kwa kupata ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Ecuador na kumaliza duru ya makundi ikiwa katika nafasi ya pili katika kundi A.

https://p.dw.com/p/4KGeS
Fußball WM 2022 Katar | Ecuador v Senegal
Picha: Aijaz Rahi/AP/picture alliance

Bila kinara wake, Sadio Mane anayeuguza jeraha, Senegal ilikuwa ya kwanza kuzitingisha nyavu za Ecuador kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Ismaila Sarr mnamo dakika ya 44 ya kipindi cha kwanza, na kuwafanya mashabiki wa Afrika kujawa na furaha kwa hali ya kipekee, mji mkuu wa Senegal Dakar ulizizima kwa shangwe na furaha.

Soma zaidi: Aliou Cisse: Timu ya Afrika itachukua Kombe la Dunia

Ecuador ilipata nafasi yake ya kutabasamu katika dakika ya 67 ya mchezo pale Moises Caicedo alipounganisha mpira wa kona na kusawazisha. Furaha ya Ecuador iliyohitaji kutoka sare tu kuweza kufuzu kwa ngwe inayofuata haikudumu kwani dakika mbili tu baadaye nahodha wa Senegal Kalidou Koulibaly alivurumusha kombora lililorejesha udhibiti wa mchezo mikononi mwao, na licha ya kujitutumua kwa uwezo wao wote, kipenga cha mwisho kilipopulizwa Ecuador walisalimu amri.

Kocha wa Senegal Aliou Cisse alisema baada ya kupoteza dhidi ya Uholanzi katika mechi ya ufunguzi, walijisikia kusukumizwa ukutani, na kwamba katika mechi ya jana walijua ni suala na kupona.

Fußball WM 2022 Katar | Ecuador v Senegal
Nahodha wa Senegal Kalidou Koulibaly akishangilia bao la ushiniPicha: Darko Vojinovic/AP/picture alliance

Uholanzi ndio imemaliza kileleni mwa kundi A, na katika mechi ya Jumanne usiku haikutaabika sana kuipiga kikumbo mwenyeji Qatar, ambayo tayari alikuwa amefungishwa virago hata kabla ya mechi hiyo.

Marekani yavuka kikwazo cha Iran

Mechi nyingine ya kufa mtu ilikuwa ile kati ya timu za Marekani na Iran, ambazo ziliingia uwanjani chini ya kiwingu cha mivutano ya kisiasa baina ya nchi zao. Iran iliianza mechi ikihitaji tu kutoka sare, huku Marekani ikilazimika kuondoka na alama zote tatu kufuzu kwa ngazi ya mtoano.

Soma zaidi: Kombe la Dunia: Brazil na Ureno zafuzu duru ya mtoano

Kila timu iliingia kwa ari kubwa, na ingawa ilikuwa bayana kuwa Marekani inaizidi Iran kiufundi, Wairan walifanya kila wawezalo kuitetea bendera ya nchi yao.

Juhudi za Marekani zilizaa matunda katika dakika ya 38 ya kipindi cha kwanza kwa goli la Christian Pulisic, goli pekee katika mtanange huo.

FIFA WM Katar 2022 | Iran v USA
Uhasama wa kisiasa pembeni: Wachezaji wa Marekani na wa Iran wakisalimiana uwanjaniPicha: Laci Perenyi/IMAGO

Rashford akunjua makucha katika ushindi wa England

England imemaliza ngazi ya makundi ikiongoza kundi B kufuatia ushindi mnono wa magoli 3-0 dhidi ya jirani wake, Wales ambayo imeambulia nukta moja baada ya mechi tatu.

Marcus Rashford aling'ara kwa kuyapachika magoli mawili huku  Phil Foden akikamilisha kwa goli la tatu. Magoli yote yaliingizwa katika nusu ya pili ya mchezo, baada ya kipindi cha kwanza kilichodorora ambapo Wales waliikatisha tamaa England kwa mbinu walizotumia kulinda lango lao.

Soma zaidi: Cameroon yaweka hai matumaini yake Kombe la Dunia

Wales walipata pigo baada ya nahodha wahe Gareth Bale kutolewa baada ya kipindi cha kwanza kutokana na jeraha.

Baada ya mbichi na mbivu kujulikana katika makundi ya A na B, England itakwaana na Senegal huku Marekani ikiweka miadi na Uholanzi.

Vyanzo: afpe, rtre