Kocha wa Ujerumani Loew apunguza wachezaji watano kikosini
8 Oktoba 2020Kocha Loew anaweka mategemeo yake katika uzoefu wa wachezaji wa Bayern Munich na RB Leizig wanaorejea katika kikosi hicho.
Ujerumani imepoteza uongozi mara tatu katika mchezo wa Uturuki na kutosheka na sare ya mabao 3-3 siku ya Jumatano, ambapo Loew alichezesha kikosi cha kujaziajazia kutokana na wachezaji wake wengi kupewa mapumziko.
Ilikuwa ni mchezo wa tatu mfululizo ambapo Wajerumani walipoteza uongozi na kumalizikia kwa sare. Pia ilikuwa ni mchezo ambao uliangaliwa na idadi ya chini kabisa ya watu katika TV katika tangu Loew aanze akiifunza timu hiyo ya taifa miaka 14 iliyopita.
Benjamin Henrichs, Nico Schulz, Niklas Stark, Nadiem Amiri na mahmoud Dahoud, ambao wote walicheza dhidi ya Uturuki, wameondolewa katika kikosi hicho kabla ya mchezo wa Jumamosi nchini Ukraine na mchezo wa nyumbani dhidi ya Uswisi siku tatu baadaye.
Wachezaji wa Bayern
Loew atakuwa na wachezaji wa Bayern Joshua kimmich, Serge Gnabry, Niklas Suele, Leon Goretzka na mlinda mlango manuel Neuer katika kikosi hicho cha wachezaji 23 baada ya kupumzishwa pamoja na Marcel halstenberg na Lukas Klostermann wa RB Leipzig.
Mshambuliaji Timo Werner , ambaye amepata nafuu kutokana na ugonjwa , pia atarejea kama ilivyo kwa mchezaji wa kati wa Real Madrid Toni Kroos.
"Itakuwa ni muhimu kushinda michezo ijayo," Loew alisema. "Kutakuwa bila shaka na timu tafauti kabisa uwanjani, kuliko dhidi ya Uturuki. Kila mmoja ana hamasa na morali ya kushinda."