Kobane wakaribia kuangukia mikononi mwa kundi la IS
7 Oktoba 2014Kuanguka kwa mji wa Kobane mikononi mwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu kutakuwa ni ushindi mkubwa kwa wapiganaji hao wa Jihad, ambao wanapigana ili kumata eneo kubwa la mpaka na Uturuki kwa ajili ya kulitangaza kuwa ni mamlaka ya Ukhalifa.
Kiasi ya watu 412, zaidi ya nusu yao wakiwa ni wapiganaji wa Jihad , wameuwawa ndani na kuzunguka mji wa Kobane tangu katikati ya Septemba, kwa mujibu wa shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria, shirika lenye makao yake makuu nchini Uingereza.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameonya kwamba mji huo muhimu kimkakati uko karibu na kuangukia mikononi mwa kundi la IS, akisema operesheni za ardhini za kijeshi zinahitajika kuweza kuwashinda wanamgambo hao.
"Ugaidi hautamalizika ...hadi pale tutakaposhirikiana katika operesheni ya ardhini," Erdogan amesema katika hotuba kwa njia ya televisheni.
Mapigano ya mitaani Kobane
Wakati mapigano kuudhibiti mji wa Kobane yakiingia katika awamu muhimu, wanamgambo wa Kikurdi wakisaidiwa na mashambulizi ya anga ya jeshi la Marekani wamepambana katika mapigano ya mitaani na wanamgambo hao wa Jihad waliokuwa wakisonga mbele, ambao wamevunja ulinzi wa mji huo jana Jumatatu.
Milio ya risasi na miripuko pamoja na ngurumo za ndege za kijeshi vilisikika kutoka upande wa mpaka wa Uturuki, wakati bendera ya Wakurdi ikionekana ikipepea katikati ya mji wa Kobane, kwa mujibu wa mwandishi habari wa shirika la habari la AFP.
"Tunahitaji msaada kutoka katika jumuiya ya kimataifa," Idris Nahsen afisa wa Kikurdi ambaye bado yuko mjini Kobane amesema . "Ama tuwamalize IS ama watatumaliza," ameongeza.
Raia watakiwa waondoke Kobane
Wapiganaji wa Kikurdi wamewaamuru raia kuondoka kutoka mji huo, baada ya wapiganaji wa Jihad kuweka bendera zao nyeusi upande wa mashariki na kuingia mjini Kobane jana Jumatatu.
Kundi la IS ni la Wasunni wenye itikadi kali , na limefadika na mparaganyiko uliotokea kutokana na makundi kadhaa nchini Syria kuingia vitani kupambana na utawala wa Syria , na wakakamata maeneo makubwa , pamoja na maeneo ya nchi jirani ya Iraw.
Kaskazini magharibi mwa Syria , wakati huo huo kundi hasimu dhidi ya Dola la Kiislamu lenye itikadi kali lenye mafungamano na al-Qaeda la Al-Nusra Front, limemkamata kasisi mmoja na Wakristo kadhaa usiku wa Jumapili, wamesema wamisionari wa Franciscana leo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman