Knesset yapitisha sheria tata ya mageuzi ya mahakama
24 Julai 2023Wabunge wa Israel wamekiridhia kipengele muhimu kwenye mpango wenye utata wa mageuzi ya mfumo wa mahakama ambao unakusudia kupunguza madaraka ya Mahakama ya Juu kwenye kupinga maamuzi wa serikali.
Kura ilipigwa muda mchache baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuwasili bungeni siku moja baada ya kutoka hospitali alikokuwa amelazwa baada ya kufanyiwa operesheni ya kuwekewa kifaa cha kudhibiti mapigo ya moyo.
Soma zaidi: Bunge la Israel lajadili muswada tata wa mageuzi ya mahakama
Kwa mujibu wa Spika wa Knesset, muswaada huo wa sheria ulipitishwa na wabunge wote 64 kutoka muungano wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia unaotawala chini ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, huku wapinzani wakisusia kura hiyo. Bunge la Israel lina viti 120.
Upinzani kutoka kila pembe
Bunge limeipitisha sheria hiyo licha ya upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na maandamano ya umma kote nchini Israel.
Tayari muungano wa vyama vya wafanyakazi, Histadrut, umesema unakutana kujadiliana uwezekano wa kuitisha mgomo wa kitaifa kufuatia kupitishwa kwa sheria hiyo bungeni.
Shirika la uangalizi wa vyama vya siasa nchini Israel, Movement for Quality Government, nalo pia limesema kwamba linakwenda mahakamani kwenda kuzuia utekelezwaji wa sheria hiyo mpya.
Soma zaidi: Bunge la Israel kupigia kura mageuzi yanayoleta mgawanyiko
Muda mchache kabla ya bunge kupiga kura, kiongozi wa upinzani, Yair Lapid, alisema kuwa juhudi za kusaka maridhiano kati yao na muungano wa vyama vinavyotawala zimeshindwa.
"Kwa serikali hii, hakuna uwezekano kabisa wa kufikia makubaliano yoyote yatakayoilinda demokrasia ya Israel. Hii ni serikali inayotaka kulipasuwa taifa, kuiharibu demokrasia, kuuchafua usalama na umoja wa watu wa Israel na mahusiano yetu ya kimataifa." Alisema kwa hasira baada ya kuchukua uamuzi wa kususia kura hiyo.
Juhudi za Rais Herzog zakwama
Awali, Rais Isaac Herzog alikuwa amejaribu kuwa mpatanishi kati ya serikali na upinzani kwa kupendekeza kuwe na muswaada wa maridhiano kwa pande zote mbili jioni ya jana, Jumapili. Lakini, ilifahamika muda mfupi baada ya mapendekezo hayo kwamba hakuna kilichoridhiwa.
Maelfu ya waandamanaji waliingia mitaani hiyo jana kuonesha shinikizo la dakika za lala salama kuzuwia mswaada huo bungeni, lakini kwa upande mwengine maelfu ya wengine waliandamana mjini Tel Aviv kuunga mkono sheria hiyo.
Soma zaidi: Netanyahu afanyiwa upasuaji wa moyo kuelekea mjadala wa bunge
Kupitishwa kwa sheria hiyo ambayo Rais Joe Biden wa Marekani ameiita "ya kugawanya" kunaelekea kutauzidisha mpasuko ndani ya taifa hilo la Mashariki ya Kati, huku waandamanaji wakiapa kuendelea na upinzani wao mitaani.
Vyanzo: dpa/AFP