1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha kupotea Jamal Khashoggi bado ni kizungumkuti

15 Oktoba 2018

Uturuki imesema serikali yake na Saudi Arabia zitatafanya ukaguzi wa pamoja katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul wiki mbili baada ya kupotea mwanahabari wa gazeti la Washington Post Jamal Khashoggi

https://p.dw.com/p/36abd
Türkei Botschaft von Saudi-Arabien in Istanbul | Protest für Freilassung von Jamal Khashoggi
Picha: Reuters/O. Orsal

Tangazo hilo la kufanya ukaguzi wa pamoja katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul limetolewa na Wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki wakati jamii ya Kimataifa ikiendelea kuwa na wasiwasi juu ya mwandishi habari Jamal Khashoggi aliepotea baada ya kuutembelea ubalozi huo tarehe 2 Oktoba.

Wabunge wa Marekani wametishia kuchukua hatua kali dhidi ya Saudi Arabia huku Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza kwa pamoja zikitoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kuaminika juu ya kisa hicho.

Türkei Istanbul Saudisches Konsulat
Polisi katika ubalozi wa Saudi ArabiaPicha: picture-alliance/AA/A. Bolat

Maafisa wa Uturuki wamesema wanahofia wauaji wa Kisaudi wamemuua Khashoggi alieandika ripoti za kumkosoa mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.

Hata hivyo taifa hilo limeyataja madai hayo kama yasiokuwa na msingi wowote lakini halijatoa ushahidi unaoonesha mwanahari huyo aliondoka kwenye ofisi hiyo ya ubalozi baada ya kuingia.

Ukaguzi unaofanyika leo ni wa kipekee kutokana na kwamba chini ya makubaliano ya Vienna maeneo ya ubalozi yanakuwa ardhi ya kigeni na yanapaswa kulindwa na nchi mwenyeji wake. Saudi Arabia huenda imekubali ukaguzi huo ufanywe ili kuwaridhisha washirika wake wa magharibi pamoja na jamii ya Kimataifa. Bado haiajawa wazi ni ushahidi gani utakaopatikana wiki mbili baada ya kupotea kwa Khashoggi.

Wafanyabiashara waanza kuususia mkutano mkubwa wa uwekezaji unaoandaliwa na Saudi Arabia

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema katika taarifa kuwa waziri wake Mike Pompeo anaelekea mjini Riyadh leo, baada ya Rais Donald Trump kusema kuwa amezungumza na Mfalme Salman kuhusu kutoweka kwa Khashoggi.

Wakati hayo yakiarifiwa wafanabiashara wakubwa wa kimataifa wameanza kujitoa katika mkutano mkubwa wa uekezaji unaojulikana kama "Davos in the Desert" au Davos Jangwani, unaoandaliwa na Saudi Arabia baadae mwezi huu.

Großbritannien Richard Branson
Mfanyabiashara tajiri wa Uingereza Richard BransonPicha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

Wafanyabiashara hao ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Uber, kampuni ambayo Saudia imewekeza mabilioni ya dola, mfanyabiashara tajiri Richard Branson, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya JPMorgan Chase  Jamie Dimon, na mwenyekiti wa kampuni ya magari ya Ford Motor Bill Ford.

Kwengineko Kuwait imesema imepinga kile inachokiita kampeni chafu dhidi ya Saudi Arabia. Naibu Waziri Mkuu wa taifa hilo Anas Al Saleh, amewataka watu kusubiri matokeo ya uchunguzi unaofanywa na maafisa husika  kuhusiana na kupotea kwa Khashoggi. Amesema Kuwait iko pamoja na Saudi Arabia kukabilianan na wale wote wenye nia ya kuhujumu mamlaka ya falme hiyo. 

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga