Kirusi kipya cha Afrika Kusini chatajwa kujibadili kwa kasi
26 Novemba 2021
Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Joe Phaahla amesema kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi ndani ya siku tano zilizopita na aina hiyo mpya ya kirusi ndio inahofiwa kuchochea kupanda kwa maambukizi. Wanasayansi nchini humo wanajaribu kutathmini ni asilimia ngapi ya visa vipya ambavyo vimesababishwa na aina mpya ya kirusi. Zaidi waziri huyo anaeleza zaidi kwamba;
"Wakati timu ya wanasayansi wakifanya utafiti na kutupa taarifa zaidi mwishoni mwa juma tutakuwa na uwezo zaidi. Lakini bila shaka, tunaona kwamba kutokana na uzoefu wa miezi 21 iliyopita au zaidi, tunaweza kutabiri jinsi hali itakavyokuwa. Kama nilivyosema, hasa wakati Delta ilivyoanza Gauteng, unaweza kuwa na uhakika kwamba watu watapoanza kutembea katika wiki chache zijazo kirusi kitakuwa kila sehemu."
Kirusi hicho aina ya B.1.1.529, pia kimeripotiwa nchini Botswana na Hong Kong miongoni mwa wasafiri waliotoka Afrika Kusini. Wataalamu wa shirika la afya duniani WHO watakutana leo kutathmini kirusi hicho na ikiwa watakipatia jina la kigiriki.
Wakati huohuo serikali ya Uingereza imetangaza kuzifuta safari za ndege kutoka Afrika Kusini na nchi nyingine tano za Kusini mwa afrika kuanzia usiku wa Ijumaa na kwamba yeyote atakayeingia kutokea katika nchi hizo atapaswa kufanya vipimo vya corona.
Waziri wa afya wa Uingereza Sajid Javid amesema kuna wasiwasi aina hiyo mpya "inaweza kuambukiza zaidi'' kuliko aina kuu ya kirusi cha delta, na kwamba chanjo zilizoko kwa sasa zinaweza kuwa na ufanisi mdogo dhidi yake. Afisa mmoja Tulio de Oliveira ambaye alifuatilia kuenea kwa kirusi cha Delta amesema aina hii mpya ya kirusi kinajibadili mara nyingi na hiyo inaweza kuchangia shinikizo kubwa katika mfumo wa afya wa Afrika Kusini ndani ya siku chache zijazo.Wanasayansi Afrika kusini wanachunguza aina mpya ya virusi vya corona
Baada ya kipindi cha maambukizi ya chini, Afrika Kusini imerekodi zaidi ya visa vipya 200 kwa siku wiki iliyopita na kufikia Jumatano maambukizi ya kila siku yaliongezeka na kupindukia 1,200. Afrika Kusini imechanja asilimia 41 ya watu wazima na inazo dozi milioni 16.5 za chanjo ya corona. Taifa hilo lenye idadi ya watu milioni 60, limerekodi zaidi ya visa milioni 2.9 vya COVID-19 na vifo ni zaidi ya 89,000.