Kiongozi wa wapiganaji ashitakiwa ICC kwa uhalifu Darfur
5 Aprili 2022Mahakama hiyo imesema kiongozi wa zamani wa kundi la wapiganaji nchini Sudan Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman, aliongoza kampeni ya mauaji, ubakaji na mateso kote katika jimbo la Darfur. Mshirika huyo wa zamani wa kiongozi aliyeondolewa madarakani nchini Sudan Omar al-Bashir, anakabiliwa na mashitaka 31 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu kutokana na jukumu lake katika mzozo huo zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Kesi yake ndio ya kwanza mbele ya mahakama hiyo ya ICC kwa uhalifu uliofanywa Darfur, ambapo zaidi ya watu 300,000 waliuawa na wengine milioni mbili na nusu wakiyahama makazi yao kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Abd-Al-Rahman anayejulikana kama Ali Kushayb na mwenye umri wa miaka 72, alikuwa kamanda mwandamizi wa kundi la Janjaweed, kundi hatari la wapiganaji lililoundwa na serikali ya Sudan, alikanusha mashitaka hayo wakati kesi hiyo ya kihistoria ilipofunguliwa.
Kesi hiyo ya ICC ni ya kukabiliana na ukatili uliofanywa na vikosi vya serikali ya Sudan katika eneo la Darfur karibu miongo miwili iliyopita. Kesi hiyo ilifunguliwa huku kukiwa na malalamiko ya kimataifa kwa ukatili unaoshutumiwa
vikosi vya Urusi katika vita vya Ukraine na ni ukumbusho kwamba Mahakama za kimataifa zinaweza kuwawajibisha watuhumiwa wa uhalifu hata kama mchakato wenyewe unaweza kuwa mrefu wenye kusuasua.
Mwendesha mashtaka Karim Khan aliita kesi hiyo kuwa "wakati muhimu wa kujaribu kuiamsha amani kutoka katika usingizi wake na kujaribu kuihamasisha kwa vitendo."