1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani auwawa Burundi

Mjahida24 Mei 2015

Kiongozi wa chama cha upinzani Burundi ameuwawa kwa kupigwa risasi, katika ghasia za hivi karibuni kwenye nchi hiyo iliokumbwa na maandamano ya wiki kadhaa, kufuatia hatua ya rais ya kuwania muhula wa tatu madarakani.

https://p.dw.com/p/1FVdb
Baadhi ya raia wa Burundi wakisimama Karibu na mwili wa kiongozi wa upinzani Zedi Feruzi
Baadhi ya raia wa Burundi wakisimama Karibu na mwili wa kiongozi wa upinzani Zedi FeruziPicha: Getty Images/AFP/C.d. Souza

Zedi Feruzi, Mkuu wa muungano wa amani na maendeleo (UPD) alikuwa akitembea akielekea nyumbani kwa miguu chini ya ulinzi wa polisi mjini Bujumbura katika wilaya ya Ngagara wakati aliposhambuliwa. Hii ni kulingana na wakaazi wa eneo hilo walioongeza kuwa mmoja kati ya maasifa watatu waliokuwa naye aliuwawa katika tukio hilo. Watu hao wasiojulikana walifanikiwa kutoroka.

Aidha muandishi habari wa shirika la AFP aliiona miili iliojaa damu ya Feruzi na mlinzi wake ikiwa nje ya nyumba ya Feruzi muda mfupi baada ya tukio hilo. Shambulio hilo lililotokea siku moja baada ya shambulizi la bomu katika soko moja mjini Bujumbura, lililosababisha mauaji ya watu watatu na wengine takriban 40 kujeruhiwa, linaongeza hali ya wasiwasi mjini humo ambako ukandamizaji mkali wa maandamano ya kuipinga serikali umewaacha watu takriban 20 wakiuwawa tangu mwezi Aprili.

"Tulisikia milio takriban ishirini ya risasi, kila mtu akalala chini, watu wakaona gari aina ya Toyota ikiondoka kwa kasi," alisema mkazi wa Ngagara, ambaye yeye mwenyewe hakushuhudia mauaji ya Feruzi. Hata hivyo afisa aliyekuwa miongoni mwa maafisa waliopewa jukumu la kumlinda kiongozi huyo wa upinzani alipata majeraha mabaya katika shambulizi hilo la risasi.

Wanajeshi wa Burundi
Wanajeshi wa BurundiPicha: Reuters/J. P. Harerimana

"Tulikuwa tunarejea kwa miguu wakati gari aina ya Toyota iliposimama karibu na sisi na wanaume waliokuwa ndani kuanza kutufyatulia risasi," alisema afisa mwengine ambaye hakutoa jina lake, alipokuwa akizungumza akiwa hospitalini. " Nilianguka sikujua kilichoendelea baadaye,"alisema afisa huyo.

Serikali yakanusha kuhusika na mauaji ya kiongozi wa upinzani Zedi Feruzi

Kwa upande wake serikali imekanusha mara moja kuhusika na kisa hicho huku ikisema imeshitushwa na mauaji hayo na kuongeza kuwa kisa hicho kinapaswa kuchunguzwa mara moja ili waliolitekeleza wakabiliwe na mkono wa sheria. Aidha shambulizi hili linaashiria kuongezeka kwa ghasia mjini Bujumbura baada ya shambulizi la bomu katika soko moja siku ya Ijumaa. Polisi imesema inamhoji mtuhumiwa wa shambulio hilo ambalo wanawalaumu waandamanaji wanaoipinga serikali kwa kulitekeleza.

Huku hayo yakiarifiwa kiongozi wa mashirika ya kiraia Vital Nshimirimana, muandaaji muhimu wa maandamano hayo ametupilia mbali madai ya polisi na kutoa wito kwa jamii ya Kimataifa kuchunguza kisa hicho. "Hatujahusika kwa aina yoyote na shambulizi hili, polisi wanajaribu kutupaka matope ili wapate sababu ya kuhalalisha mauaji ya waandamanaji," alisema Nshimirimana

Huku hayo yakiarifiwa kiongozi mwengine wa mashirika ya kiraia Pacifique Nininahazwe, siku ya ijumaa alitangaza kusitisha maandamano kwa siku mbili ili kutoa nafasi ya watu kuwazika kwa heshima wale waliouwawa wakitetea demokrasia nchini mwao. Lakini akaonya kuwa maandamano yataanza tena siku ya Jumatatu yakiwa na nguvu mpya.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi Pierre NkurunzizaPicha: Reuters/G. Tomasevic

Mazungmzo ya siri kati ya upinzani na serikali yanaendelea Bujumbura

Hata hivyo katika tangazo la kutia moyo kiongozi huyo wa moja ya mashirika ya kiraia alisema mazungumzo ya siri yameanza kufanyika kati ya waandamanaji, vyama vya upinzani pamoja na serikali.

Majadiliano hayo yameungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na mataifa jirani. Mgogoro wa kisiasa nchini Burundi ulianza mwishoni mwa mwezi Aprili, baada ya chama tawala cha CNDD FDD kuteua rais Nkurunziza kugomea tena katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 mwezi Juni.

Mzozo huo ulipanuka zaidi wiki iliopita baada ya jenerali mkuu wa jeshi Godefroid Niyombare kutangaza mapinduzi yalioshindwa dhidi ya serikali ya Nkurunzinza. kufuatia hali hiyo Uchaguzi wa bungeuliotarajiwa kufanyika Mei 26 umefutiliwa mbali kwa wiki moja na sasa unatarajiwa kufanyika tarehe 5 mwezi Juni.

Aidha upinzani na mashirika ya kutetea haki za binaadamu wanasema kwamba hatua ya Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu kwa miaka mitano inakiuka katiba ya nchi, na makubaliano ya amani yaliomaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliodumu kwa takriban miaka 13.

Baadhi ya waandamanaji wanaompinga rais Pierre Nkurunziza
Baadhi ya waandamanaji wanaompinga rais Pierre NkurunzizaPicha: Getty Images/AFP/C. De Souza

Nkurunziza, kiongozi wa zamani wa waasi na mkristo aliyeokoka anayeamini kuwa anaungwa mkono na Mwenyezi Mungu katika uongozi wake anatoa hoja kwamba kipindi cha kwanza hakipaswi kuhesabiwa kwa sababu aliteuliwa na bunge na wala hakuchaguliwa na wananchi kama katiba inavyosema.

Kwa upande mwengine wakimbizi wanaendelea kuikimbia nchi hiyo, wengi wao wakiingia nchi jirani ya Tanzania ambako zaidi ya watu 50,000 wanajaribu kujikimu kimaisha katika mazingira magumu katika mwambao wa mto Tanganyika.

Ugonjwa wa kipindupindu umeripotiwa kuripuka katika baadhi ya makambi ya wakimbizi huku watu 31 wakiripotiwa kufariki kutokana na mripuko huo miongoni mwa watu 3000 walioambukizwa ugonjwa huo huku idadi ikizidi kupanda kufikia watu 400 kwa siku hii ikiwa ni kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi.

Mwandishi: Amina AbubakarAFP/Reuters/AP

Mhariri: Sekione Kitojo