Kiongozi wa chama cha upinzani atekwa nyara Chad
22 Septemba 2024Chama cha upinzani nchini Chad kimedai kiongozi wake ametekwa nyara na maafisa wa ujasusi baada ya kuwa na mkutano na baadhi ya wanachama wa upinzani.
Chama cha upinzani cha PSF kimesema kiongozi wao huyo Robert Gam ambaye ni katibu mkuu wa chama ndiyo kiongozi wa hivi karibuni wa chama hicho kuangukia kwenye hujuma za watawala wa kijeshi nchini Chad.
Taarifa za kutekwa kwa mwanasiasa huyo zimetolewa na mratibu mkuu wa chama Mahamat Alifa Yousouf ambaye alitowa taarifa hiyo kwa shirika la habari la AFP siku ya Jumamosi.
Amesema kwamba kiongozi huyo alitoweka mara baada ya kutembelewa na wanachama wa chama cha upinzani cha Wazalendo katika makao makuu ya chama cha PSF.
Mwanasiasa huyo wa upinzani amekuwa akiandamwa na matukio ya unyanyasaji na vitisho tangu kuuwawa kwa mgombea urais wa chama chake Yaya Dillo Djerou mwezi Februari, na wanaoaminika kuwa jeshi.
Naibu wa Gam, ambaye ni Fatime Adoume Youssouf aliwaambia waandishi habari Jumamosi usiku kwamba magari matatu yaliyokuwa hayana nambari za usajili yakiwa na vioo vyeusi pamoja na pikipiki chungunzima zilizoonesha kutia shaka,zilionekana karibu na eneo ulikokuwa ukifanyika mkutano siku ya Ijumaa.
Fatime anasema ni wazi kwamba katibu mkuu wa chama chake Robert Gam alitekwa nyara na maafisa wa ujasusi.Ikumbukwe kwamba aliyekuwa mgombea wa chama hicho cha PSF aliuwawa wakati wa shambulio lililofanywa dhidi ya ofisi za makao makuu ya chama hicho na walinzi wa rais wa Chad,ikiwa ni miezi miwili kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais uliopita.
Kwa mujibu wa upinzani Dillo aliuwawa kwa kupigwa risasi ya kichwa.Hata hivyo jeshi la Chad lilikanusha kuhusika na mauaji yoyote likidai kwamba lilihitaji kumkamata Dillo kwa tuhuma za kuhusika na shambulizi dhidi ya idara za ujasusi nchini humo,kwa lengo la kutaka kuachiliwa huru kwa kiongozi wa chama chake.Soma pi: Chad iko katika hali ya tahadhari baada ya shambulizi kwenye idara ya usalama
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ikiwemo Amnesty International yamesema viongozi wengi wa upinzani nchini Chad wamekamatwa na wanazuiliwa na vikosi vya usalama bila ya kufuatwa sheria.
Pamoja na kwamba aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha upinzani cha PSF Yaya Dillo alikuwa ni hasimu mkubwa wa kisiasa wa rais Mahamat Idris Deby Itno,walikuwa pia ni mtu na binamu yake.
Mahamat Deby alitangazwa kuchukua kiti cha uongozi wa nchi na jeshi Aprili mwaka 2021 pale baba yake Idriss Deby Itno alipouwawa na waasi baada ya kukaa madarakani kwa miaka 30.
Mwezi Mei mwaka huu 2024 Mahammat Deby akashinda uchaguzi wa rais,uliosusiwa na upinzani na waangalizi wa kimataifa walisema haukuwa uchaguzi wa haki wala wa kuaminika.