Aung San Suu Kyi apunguziwa kifungo kwa miaka sita
1 Agosti 2023Kulingana na msemaji wa jeshi Zaw Min Tun, miaka hiyo imeondolewa katika kifungo chake baada ya tangazo kwamba amesamehewa katika kesi tano zinazomkabili. Kiongozi huyo wa zamani bado anakabiliwa na kesi 14 licha ya msamaha huo wa jeshi. Kumekuwa na hofu kuhusiana na hali ya kiafya ya Suu Kyi aliyewahi kushinda tuzo ya Nobel na wiki iliyopita jeshi lilimhamisha kutoka jela na kumpeleka katika jengo la kiserikali.
Rais wa zamani, Win Myint, pia kupunguziwa kifungo chake
Baada ya mapinduzi ya Februari Mosi 2021, jeshi la Myanmar lilimuondoa madarakani Suu Kyi aliyechaguliwa kidemokrasia. Baadaye mahakama ya kijeshi ya nchi hiyo ilimhukumu jumla ya miaka 30 jela kwa madai ya mashtaka ya jinai. Jeshi limesema rais wa zamani, Win Myint, ambaye pia alihukumiwa miaka mingi jela, naye atapunguziwa kifungo chake.