Kiongozi wa makumbusho ya Yad Vashem kuizuru Ujerumani
18 Januari 2023Mkuu wa makumbusho ya mauaji ya halaiki dhidi ya Wayahudya Yad Vashem nchini Israel, Dani Dayan anatarajiwa kufanya ziara nchini Ujerumani, ya kwanza maishani mwake.
Katika mahojiano maalumu na DW Dayan amesikitika kwamba chuki dhidi ya Wayahudi imeenea tena duniani. Amesema hiyo ndio sababu huwa anawahimiza viongozi wa dunia wanaoyatembelea makumbusho ya Yad Vashem kuchukua hatua za haraka mara tu waonapo dalili za chuki dhidi ya Wayahudi, kwa kuwa wakichelewa chuki hiyo itafika katika kiwango kisichoweza kudhibitiwa.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa makumbusho ya Holocaust amesema hali ya leo ni tofauti na ya miaka 80 iliyopita, kwa sababu hivi sasa watu wanatambua hatari inayoweza kutokea, akasisitiza lakini jukumu la kila mmoja katika kupinga chuki dhidi ya Wayahudi, ubaguzi wa rangi na kutovumiliana.