1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Kiongozi wa Kashmir aliyepigania kujitenga azikwa

2 Septemba 2021

Kiongozi wa kundi la watu wanaotaka kujitenga katika jimbo lenye mzozo la Kashmir Syed Ali Geelani amezikwa alfajiri ya Alhamisi wakati mamlaka za India zikiweka marufuku ya kutembea katika eneo lote la Himalaya.

https://p.dw.com/p/3zpbK
Kaschmir Syed Ali Shah Geelani Separatistenführer
Picha: Altaf Qadri/AP Photo/picture alliance

Mwanaharakati huyo aliyesimama kuupinga utawala wa India katika jimbo la Kashmir alifariki siku ya Jumatano tarehe 01.09.2021 akiwa na umri wa miaka 92 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya moyo na figo.

Kwa kuhofia machafuko kutokana na ushawishi wake, vikosi vya usalama vilipelekwa haraka katika jimbo la Kashmir, mtandao wa Interneti na simu zilikatwa na wakaazi walitakiwa kubaki majumbani mwao. Walinda usalama waliweka vizuizi siku nzima na amri ya kutotoka nje inatarajiwa kuongezwa hadi baada ya maombolezo ya jadi za kwa familia yatakapokamilika hapo siku ya Jumapili.

Hata hivyo familia ya Geelani wamesema hawakuruhusiwa kuhudhuria mazishi yaliyofanyika saa kumi na nusu alfajiri kwenye makaburi yaliyo karibu na nyumbani kwake katika jiji la Srinagar.

Geelani, ambaye kwa mua wa zaidi ya miongo mitano alikuwa gerezani au mara nyingine chini ya kifungo cha nyumbani, alitaka kuzikwa kwenye Makaburi ya Mashahidi ya Srinagar pamoja na wanaharakati wengine waliopigania kujitenga kwa jimbo la Kashmir lakini mamlaka ilikataa ombi hilo.

Indien Kaschmir Polizei Militär Oppositionsführer Syed Ali Shah Geelani
Polisi wa India walifanya doroa kali Picha: Mukhtar Khan/AP Photo/picture alliance

Mwanawe, Naseem Geelani, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba walisisitiza kumzika baada ya sala ya alfajiri katika makaburi hayo ya mashahidi kulingana na matakwa yake lakini amesema polisi waliunyakua mwili wa baba yake na hawamkuruhusu mtu yeyote kutoka kwenye familia kushiriki kwenye mazishi.

Kifo cha kiongozi huyo wa kundi la watu wanaotaka kujitenga katika jimbo lenye mzozo la Kashmir kimeongeza mgawanyiko katika mzozo huo. Hali nyingine inayoongeza mafuta kwenye mzozo huo ni misako ya serikali ya India inayolenga kufuatilia nyendo za watu na kubana mawasiliano, hayo yote yanaangazia machafuko na mgogoro unaotokota chini kwa chini kwenye eneo linalozozaniwa la Kashmir.Je Umoja wa mataifa hautaki kuingilia kati mgogoro wa Kashmir?

Kwa wengi katika eneo hilo, Geelani alikuwa uso wa Kashmiri katika upinzani dhidi ya India. Kwa wakosoaji wake, alikuwa muhafidhina aliyesababisha mivutano katika jimbo hilo, madai ambayo aliyakanusha wakati wote wa uhai wake.

Karibu watu 50 walihudhuria mazishi, kulingana na mtu mmoja ambaye alisema alikuwa jirani ya Geelani. Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutoa salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Geelani. Geelani alikuwa kama mwiba kwa India tangu mwanzoni mwa miaka ya 60 alipoanza kufanya kampeni ya kutaka eneo lenye waislamu wengi la Kashmir upande wa India liungane na upande unaodhibitiwa na Pakistan.