1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa IS Al-Baghdadi aibuka katika mkanda wa sauti

29 Septemba 2017

Habari za kifo cha kiongozi wa Dola la Kiislamu Abu Bakri Al-Baghdadi zitaonekana zilitiwa chumvi, ikiwa mkanda mpya wa sauti yake utathibitiwa. Katika mkanda huo, anawataka wafuasi wake kuendeleza vita dhidi ya maadui.

https://p.dw.com/p/2kwvK
Abu Bakr al-Baghdadi Führer Islamischer Staat
Picha: Getty Images/AFP

Kituo cha habari cha kundi hilo la Dola la Kiislamu hapo jana kimetoa mkanda wa sauti inayodaiwa kuwa ya Al-Baghdadi, akiapa kuendeleza mapambano na kuwamuagia sifa wapiganaji wa kundi hilo kwa ujasiri wao katika uwanja wa vita - licha ya wanamgambo hao kuupoteza mji wa kaskazini mwa Iraq wa Mosul mwezi Julai.

Katika mkanda huo wa dakika 46, Al-baghdadi anawatolea mwito pia wafuasi wake kufanya mashambulizi dhidi ya mataifa ya Magharibi na kuendeleza mapambano nchini Iraq, Syria na kwingineko.

"Enyi wanajeshi wa Kiislamu, wafuasi wa Khilafa popote mlipo, zidisheni mashambulizi na vijumuisheni vituo vya habari vya makafiri na makao makuu ya vita vyao vya kiitikadi miongoni mwa shabaha zenu," alisema Al-Baghdadi.

Abu Bakr al-Baghdadi Bildnis in Flammen
Waandamanaji wa Kishia wakichoma picha ya Al-Baghdadi wakati wa maandamano mjini New Delhi, India, Juni 9, 2017. Ilikuwa baada ya kundi la IS kudai kuhusika na mashambulizi mawili dhidi ya bunge la Iran na kaburi la kiongozi wa Mapinduzi ya Iran.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Swarup

"Endelezeni jihadi yenu na mshambulizi yenu yaliobarikiwa, na msithubutu kuwaruhusu wapiganaji wa vita vya msalaba na waasi wa dini kufurahia maisha nyumbani wakati ndugu zenu wanakabiliwa na mauaji, mashambulizi na uharibifu."

Urusi ilidai kumuuwa mwezi Juni

 

Maafisa wa Urusi walisema mwezi Juni kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba al-Baghdadi aliuawa katika shambulio la ndege za Urusi nje ya mji wa Syria wa Raqqa, ambao ndiyo ngome kuu ya kundi. Baadae maafisa wa Marekani walisema wanaamini bado yuko hai.

Mahaka alipo al-Baghadadi hapajulikani lakini anaaminika kuwa katika maeneo yanayozidi kupungua ya IS mashariki mwa Syria. Miji inayoshikiliwa na IS ya Raqqa na Deir al-Zour iko chini ya mzingiro na yumkini ni hatari sana kwake kujificha huko.

Baadhi ya viongozi wa IS wanaaminika wamekwenda kujificha katika mji wa karibu wa Mayadeen, nakundi hilo bado linadhibiti sehemu ya Mto Euphrates kuanzia Deir al-Zour hadi kwenye mpaka wa Iraq, na pia maeneo ya jangwa ya mpakani.

Al-Baghdadi aliwasifu pia wapiganaji wake kwa kile alichokiita mapambano ya kijasiri dhidi ya vikosi vya Iraq vinavyoungwa mkono na Marekani vilivyowafurusha kutoka mji wa Mosul, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini humo, baada ya karibu miezi tisa ya mapambano.

Awatahadharisha Wasunni wa Syria

Katika ukanda huo, aliwapa pole pia wapiganaji kwa vipigo kadhaa walivyovipata katika uwanja wa vita katika miezi ya karibuni nchini Iraq na Syria, huku pia akiwatolewa mwito wa kutosalimu kamwe. Akiwahutubia Wasunni walio wengi nchini Syria, amewaonya dhidi ya ujanja wa wa Alawi walio wachache, ambao ni tawi la madhehebu ya Kishia anakotokea rais wa Syria Bashar al-Assad, na pia dhidi ya mbinu za Uturuki, na washirika wa Assad, Urusi na Iran.

Irak Ruinen von Mosuls Geburtsklinik
Sehemu kubwa ya mji wa Mosul ilibaki magofu baada ya vita vya karibu miezi tisa kuwandoa wapiganaji wa ka IS katika mji huo.Picha: Reuters/A. Lashkari

Al-Baghdadi pia alizungumzia kile alichokiita ushawishi wa Marekani unaozidi kupungua duniani, na kusema Urusi ilikuwa inatumia mwanya huo kujitanabahisha kama taifa lenye nguvu zaidi kuchukuwa nafasi ya Marekani. Amesema Urusi ndiyo ina udhibiti kamili wa Syria.

Katika mkanda huo, Al-Baghdadi amesem kipaumbele cha Waislamu ni kumridhisha Mwenyezi Mungu, na kwamba ushindi dhidi ya adui wa Mwenyezi Mungu unafuata baada ya hilo.

Katika kilele chake mwaka 2014 - wakati jeshi la Iraq liliposambaratika mbele ya mashambulizi ya wanamgabo hao - IS ilidhibiti theluthi moja ya Syria na Iraq lakini imekuwa ikipoteza maeneo yake kufuatia mashambulizi ya muungano unaoongozwa na Marekani, ambao umeyasadia majeshi ya Iraq, na vile vile wapiganaji wanaoongozwa na Wakurdi wanaopambana na wanamgambo hao nchini Syria.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape, rtre, dpae

Mahriri: Daniel Gakuba