Kiongozi wa Belarus atishia kutumia silaha za nyuklia
27 Septemba 2024Kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenkoleo ametishia kutumia silaha za nyuklia baada ya kuituhumu Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuwa na mipango ya kuivamia nchi yake.
Akizungumza kwenye hadhara iliyokusanya wanafunzi mjini Minsk, mtawala huyo wa moja ya mataifa yaliyokuwa sehemu ya Dola ya Kisovieti, amesema shambulio lolote dhidi ya Belarus litamaanisha kuwa ni mwanzo wa Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia.
Amesema nchi yake pamoja na mshirika wake wa karibu Urusi, hawatasita kutumia silaha za nyuklia na amempongeza Rais Vladimir Putin kwa uamuzi wake wa hivi karibuni wa kubadili masharti yatakayoilazimisha Moscow kutumia silaha hizo za maangamizi.
Mapema wiki hii Rais Putin alisema Urusi inaweza kutumia silaha za nyuklia hata dhidi ya nchi inayoungwa mkono kijeshi na dola lenye nguvu za nyuklia. Msimamo huo ulizusha hamkani na ukosoaji kutoka Ukraine ambayo inaungwa mkono kijeshi na madola yenye silaha za nyuklia hususani Marekani.