Kinyan'ganyiro kikali cha uchaguzi wa Rais Tanzania
24 Oktoba 2015Rais Jakaya Kikwete anayeondoka madarakani ambaye hagombei kutokana na kutumikia mihula miwili inayoruhusiwa kikatiba ameliamuru jeshi la polisi kuimarisha usalama ili kuhakikisha kwamba upigaji kura kwa wananchi takriban milioni 53 unafanyika kwa amani.
John Magufuli wa chama cha mapinduzi (CCM) kilichotawala kwa muda mrefu nchini Tanzania ambaye anawekewa matumaini ya kushinda uchaguzi huo amesema katika mojawapo ya hotuba zake za mwisho " Nataka kuongoza nchi kuelekea kwenye maendeleo na ustawi wa jamii."
Amesema "Kila mtu anastahiki maisha bora bila ya kujali itikadi yake ya kisiasa."
Wasi wasi wa ghasia
Lakini watu wengi wanaamini kwamba Magufuli mwenye umri wa miaka 55 atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Edward Lowasa waziri mkuu wa zamani mwenye umri wa miaka 62 ambaye anaongoza muungano wa vyama vinne vya upinzani vilivyounda UKAWA umoja wa katiba ya wananchi. Lowasa amekiasi chama chake cha CCM hivi karibuni na kujiunga na CHADEMA.
Lowasa amesema "Tuin'gowe madarakani CCM utawala ambao umeliangusha taifa kwa miaka 54 ya kuwa madarakani. "
Mwanasiasa mkongwe Pius Msekwa ambaye ni makamo mwenyekiti wa zamani wa chama CCM na makamo kansela wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema uchaguzi huu utakuwa mgumu na wenye hamasa kubwa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nchi.
Wachambuzi wanaonya kwamba kutokana na uchaguzi huu kuwa mkali ambalo sio jambo la kawaida kwa upinzani kutowa ushindani wa kuaminika kwa CCM tokea kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi hapo mwaka 1995 kunaweza kukazuka mvutano.
Kushindwa kwa heshima
Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan ambaye anaongoza timu ya waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Madola amesema wiki hii " Iwapo unashindwa kubali kushindwa."
"Jiandae kushindwa kwa heshima " huu ni wito uliotolewa na gazeti la Tanzania Citizen wiki hii katika uhariri wake na kukumbusha kwamba "maisha daima yaendelee baada ya uchaguzi."
Wagombea wote wawili Magufuli na Lowasa wamekuwa wakitowa wito mara kwa mara wa kudumishwa kwa amani na umoja wa kitaifa katika hotuba zao ambazo zimeshutumu rushwa na vurugu kwa misingi ya kikabila na dini.
Benki ya Dunia inasema licha ukuaji wa kiuchumi wa kupigiwa mfano wa nchi hiyo wananchi wengi hawakufaidika na hilo na nchi hiyo inaendelea kuwa ya kimaskini kabisa kwa kuzingatia viwango vya kanda na vya kimataifa.
Zanzibar kumchaguwa rais wao
Mbali na uchaguzi wa rais wapiga kura pia watachaguwa wabunge na madiwani wa serikali za mitaa katika uchaguzi huo wa Jumapili ikiwa ni pamoja na uchaguzi wa visiwa vya Zanzibar vyenye mamlaka fulani ya kujiamulia mambo yake ambavyo vitamchaguwa rais wao mwenyewe.
Visiwani Zanzibar kampeni kwa kiasi kikubwa zimefanyika kwa amani lakini wakaazi wamekuwa wakiweka ndani akiba ya chakula na maji wakihofia kuzuka kwa ghasia baada ya uchaguzi huo.
Rais wa visiwa hivyo na makamo wake ambao wanaongoza serikali ya umoja wa kitaifa watachuana vikali kuwania urais wa visiwa hivyo ambavyo wapiga kura wake zaidi ya 500,000 wanatarajiwa kuteremka vituoni kupiga kura zao.
Wagombea hao wakuu ni Rais Ali Mohamed Shein wa chama tawala cha CCM na makamo wa kwanza wa rais Seif Sharif Hamad kutoka chama cha upinzani cha CUF wanaoshirikiana madaraka katika serikali ya umoja wa kitaifa.
Hali hadi sasa hali ni shwari ingawa Umoja wa Mataifa pia umetowa angalizo kwa wafanyakazi wake kwamba kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura kuwa vijana haiwezi kutabiri jinsi watakavyosheherekea ushindi au kuhuzunika na kushindwa.Imewataka wafanyakazi wake kuwa macho na kuweka akiba ya chakula na maji na imeyataja maeneo ambayo yumkini yakazuka vurugu baada ya kutangazwa kwa matokeo kuwa ni Dar es Salaam, Zanzibar,Mbeya,Mwanza na Arusha.
Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP
Mhariri : Bruce Amani