Kimbunga Daniel chaua watu zaidi ya 2,000 Libya
12 Septemba 2023Waziri anayehusika na usafiri wa anga wa Libya ambaye pia ni mwanachama wa kamati ya dharura, Hichem Chikiouat amesema zaidi ya miili 1,000 imeopolewa katika mji wa Derna mashariki mwaLibya kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Daniel kutoka barahari ya Mediterania.
Waziri huyo amesema amerejea kutoka mji wa Derna, hali ni mbaya inatisha na miili imezagaa kila mahali - baharini, kwenye mabonde na hata chini ya majengo, na anatarajia idadi ya vifo itaongezeka sana na kuwa kubwa mno.
Amesema asilimia 25 ya mji huo imetoweka na majengo mengi sana yameanguka.
Msemaji wa majeshi ya mashariki mwa Libya Ahmed al-Mosmari, amesema idadi ya vifo mjini Derna, imepita 2,000, na kuna watu kati ya 5,000 na 6,000 ambao hawajulikani waliko.
Al-Mosmari amesema janga hilo limesababishwa na kuanguka kwa mabwawa mawili yaliyo karibu, na kusababisha mafuriko makubwa ya ghafla.
"Katika mji wa Derna pekee kuna watu zaidi ya 2,000 waliokufa na tunaziombea roho zao. Bado kuna maalfu ya watu ambao hawajulikani waliko mjini humo na idadi hii inaweza kuongezeka kwa kiwango kikubwa. Mabwawa yalianguka kusini mwa Derna. Madaraja matatu yalianguka kabisa na maji yakasambaa kwenye vitongoji na kuna vitongoji vizima ambavyo vimesombwa na kuingia baharini, wakiwemo wakazi wao."
Msaada wapelekwa mashariki mwa Libya
Mkuu wa serikali ya Umoja wa kitaifa ya Libya, Abdulhamid al-Dbeibah, ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba ndege ya dharura iliyobeba tani 14 za mahitaji, dawa, vifaa.
mifuko ya kuwekea maiti pamoja na maafisa 87 wa afya inaelekea mji wa Benghazi kusaidia maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.
Mkuu wa ujumbe wa Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu na hilal nyekundu IFRC nchini Libya Tamer Ramadan amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwa njia ya video akiwa nchini Tunisia kwamba idadi ya vifo kutokana na mafuriko huenda ikaongezeka kufikia maalfu.
Ramadan aidha amesema idadi ya watu ambao hawajulikani waliko imefikia 10,000.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema idadi ya juu ya vifo na majeruhi inatarajiwa kufuatia mafuriko mashariki mwa Libya.
Scholz amesema Ujerumani inasimama pamoja na Umoja wa Mataifa na washirika wengine kuhusu uwezekano wa kupeleka msaada Libya.
Umoja wa Ulaya unaipelekea Libya msaada kufuatia kimbunga Daniel.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Josep Borell ameandika katika mtandao wa X akisema Umoja wa Ulaya unafualia kwa karibu hali inayoendelea nchini Libya na iko tayari kutoa msaada.
Borell amesema amesikitishwa na picha za uharibifu Libya ambayo inayokabiliwa na hali mbaya ya hewa inayosababisha huzuni kubwa ya kuangamia kwa maisha ya watu wengi.
Mjumbe maalum wa Marekani kwa ajili ya Libya amesema Marekani itaidhinisha msaada kwa Libya baada ya nchi hiyo kuomba isaidiwe.