1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Beryl chasababisha uharibifu jimboni Texas

9 Julai 2024

Kimbunga Beryl kimepiga jimbo la Texas jana Jumatatu na kusababisha kukatika kwa nguvu za umeme katika takriban nyumba milioni 3 na biashara na pia kusababisha mvua kubwa

https://p.dw.com/p/4i26X
Mti waangukia gari jimboni Texas baada ya eneo hilo kukumbwa na kimbunga Beryl mnamo Julai 8 2024. Kimbunga hicho kimesababisha vifo vya watu wawili.
Mti waangukia gari jimboni Texas baada ya eneo hilo kukumbwa na kimbunga BerylPicha: Mark Felix/AFP/Getty Images

Maafisa jimboni Texas pamoja na wale wa serikali, wameonya kuwa huenda ikachukuwa siku kadhaa kurejesha nguvu za umeme baada ya kimbunga hicho kufika ufukweni kikiwa katika ngazi ya kwanza ya ukubwa katika kipimo kinachotumiwa kupanga kitisho cha vimbunga na kukata nyaya za umeme pamoja na kuangusha miti.

Soma pia: Kimbunga Beryl chahama kuelekea Houston

Baada ya saa chache, kimbunga hicho kilikuwa kimepungua makali na kuwa cha kitropiki, kikiwa na nguvu ndogo kuliko kile cha ngazi ya 5 kilichosababisha uharibu mkubwa katika sehemu za Mexico na Karibea wikendi iliyopita.

Watu wawili wauawa baada ya miti kuangukia nyumba 

Takriban watu wawili waliuawa wakati miti ilipoangukia nyumba, huku Kituo cha Kitaifa cha kufuatilia Vimbunga cha nchini Marekani (NHC) kikisema upepo mbaya na mafuriko ya ghafla yataendelea huku kimbunga Beryl kikielekea katika eneo la bara.

Hata hivyo hakukuwa na ripoti za haraka kuhusu uharibifu wa miundo mbinu.