Kifo cha mgombea urais, Ecuador yatangaza hali ya tahadhari
10 Agosti 2023"Kuanzia sasa jeshi limeamrishwa kuhakikisha usalama kwa raia, utulivu wa nchi na uchaguzi huru na wa kidemokrasia mnamo Agosti 20 kama ilivyopangiwa na Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi. Ni sharti tuungane pamoja leo zaidi ya siku nyengine yoyote ile na tuwe na uhakika kwamba tunaweza kukabiliana na chuki. Mungu ibariki Ecuador," alisema Lasso.
Hali hiyo ya tahadhari aliyoitangaza baada ya kukutana na baraza lake la mawaziri, itadumu kwa kipindi cha siku 60. Rais huyo pia ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
Mshukiwa wa mauaji hayo afariki dunia
Vyombo vya habari nchini Ecuador vinaripoti kuwa watu wasiojulikana walimfyatulia risasi mgombea urais Fernando Villavicencio alipokuwa akiabiri gari baada ya mkutano wa kampeni mjini Quito.
Afisi ya mwanasheria mkuu katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini imesema mshukiwa mmoja amejeruhiwa vibaya katika ufyatulianaji risasi na maafisa wa usalama, na baadae akafariki dunia alipokuwa akipelekwa hospitali.
Rais Lasso amesema watu sita tayari wamekamatwa kufuatia tukio hilo ambalo amelitaja kama uhalifu wa kisiasa uliokuwa na dalili za ugaidi.
Waendesha mashtaka wamesema watu tisa walijeruhiwa katika tukio hilo akiwemo mgombea wa ubunge na maafisa wawili wa polisi.
Villavicencio alimfungulia mashtaka rais wa zamani
Villavicencio alikuwa mgombea urais wa Vuguvugu la Build Ecuador na katika kura za maoni za hivi karibuni alishika nafasi ya nne wakati mmoja na nafasi ya tano katika kura nyengine.
Kama mwandishi wa habari na mbunge, Villavicencio aliukosoa mara kwa mara ufisadi uliokithiri nchini Ecuador. Aliwafungulia kesi nyingi maafisa katika serikali ya rais wa zamani Rafael Correa aliyeiongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 2007 hadi 2017. Wakati mmoja alimfungulia kesi rais Correa mwenyewe.
Rais wa sasa Guillermo Lasso alikuwa amelivunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema wakati ambapo bunge, lilikuwa linaendelea na vikao vya kumuondoa madarakani rais huyo kutokana na madai ya ubadhirifu wa fedha yaliyokuwa yanamkabili.
Ecuador iko katika mgogoro wa kisiasa huku kiwango cha imani dhidi ya serikali na bunge kikiwa chini mno. Uhalifu nchini humo umeongezeka pakubwa katika siku za hivi karibuni kutokana na kuingia kwa wingi nchini humo kwa walanguzi wa madawa ya kulevya, huku kiwango cha mauaji kikiwa juu zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Vyanzo: DPAE/AP/Reuters