1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khamenei aapa kuishambulia tena Israel, Marekani yaonya

3 Novemba 2024

Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ametangaza kuwa Iran italipiza kisasi dhidi ya Israel kufuatia mashambulizi yake, huku Marekani ikiionya Tehran kwamba haizaizuwia Israel ikiwa itashambulia

https://p.dw.com/p/4mXfj
Iran | Ayatollah Ali Khamenei
Kiongozi wa Juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameapa kuiadhibu Iran kwa mashambulizi yake ya Oktoba 2024.Picha: Iranian Leader Press Office/Anadolu/picture alliance

Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ametangaza kuwa Iran itachukua hatua za kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Israel, huku mjumbe wa kijeshi wa Israeli akithibitisha kukamatwakwa mtendaji mmoja wa Hezbollah katika uvamizi wa Lebanon.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema watoto wanne ni miongoni mwa watu sita waliokolewa katika shambulizi kwenye kituo cha chanjo ya polio kaskazini mwa Gaza, ambapo mashirika ya UN yameeleza hali kuwa ni "mbaya sana" kutokana na mashambulizi makali ya Israeli.

Khamenei alionya kuwa Iran itajibu mashambulizi dhidi yake na washirika wake. Aidha, tarehe 26 Oktoba, Israel ilifanya mashambulizi kwenye maeneo ya kijeshi nchini Iran, na kuua wanajeshi wanne.

Soma pia: Israel yafanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran

Wakati huo huo, Marekani imetangaza kupeleka ndege zake za kivita B-52 katika Mashariki ya Kati huku ikiionya Tehra dhidi ya kuishambulia tena Israel.

Gazeti la Axios limewanukuu maafisa wa Marekani wakisema Washington haikuwa na uwezo wa kuizuwia Israel endapo itashambuliwa tena na Iran.

Iran | Gwaride la Kijeshi mjini Tehran
Iran inatumia mifumo ya ulinzi wa anga iliyotengenezwa nchini Urusi, aina ya S-300.Picha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Gaeti hilo lilisema duru za Marekani na Israel zimesema Iran ilikuwa inajiandaa kuishambulia tena Israel katika siku zizajo, mkabla ya uchaguzi wa Novemba 5.

Tangu mwishoni mwa Septemba, Israel imekuwa katika vita kamili dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon, huku pia ikipambana na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza. Israeli imefanya mashambulizi makali katika eneo la Jabalia, na WHO imesema watu 50, wakiwemo watoto, wameuawa katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita.

Soma pia: Misri yapendekeza kusitishwa mapigano kwa siku mbili Gaza

Hadi sasa, takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 43,000 wameuawa katika Gaza tangu kuanza kwa operesheni za kijeshi za Israeli. Nchini Lebanon, uvamizi wa Israeli umesababisha vifo vya watu 1,930 tangu kuanza kwa vita.

Msemaji wa serikali ya Lebanon amesema kuwa uvamizi huo umepelekea maelfu ya watu kuhama makwao, huku wakazi wakikabiliwa na uhaba wa mahitaji ya msingi.

Waziri mkuu wa Lebanon, Najib Mikati, ameagiza kuwasilisha malalamiko kwa Baraza la Usalama la UN kuhusu uvamizi wa Israel katika mji wa Batroun.