Kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel ICJ inahusu nini?
10 Januari 2024Katika wasilisho lenye kurasa 84, mbali na mambo mengine, Afrika Kusini inasema kuwa kwa kuwauwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, Israel imewasababishia madhara makubwa ya kiakili na kimwili na kufanya hali ya maisha kuwa ngumu, katika kiwango kinachohesabiwa kuwa sawa na "mauaji ya halaiki" dhidi ya Wapalestina.
Afrika ya Kusini inaituhumu Israel kwa kushindwa kufikisha mahitaji ya kiutu katika Ukanda wa Gaza yakiwemo maji, chakula, dawa na misaada mingine ya kibinadamu katika vita vyake na Hamas vilivyodumu kwa zaidi ya miezi mitatu.
Pia inataja kampeni endelevu ya uripuaji wa mabomu kiholela ambayo imeharibu sehemu kubwa ya eneo hilo, kulazimisha kuhamishwa kwa takriban Wapalestina milioni 1.9 na kuua zaidi ya watu 23,000 kulingana na mamlaka ya afya Gaza.
Wasilisho la Afrika Kusini linaongeza kuwa katika vitendo vyote Israel ilivyohusishwa, ilishindwa kuzuia mauaji na hivyo kukiuka Mkataba wa Geneva juu ya Mauaji ya Halaiki.
Pia Afrika kusini inaishutumu Israel kwa kushindwa kuzuia uchochezi wa mauaji ya halaiki kwa maafisa wake na hivyo kuiomba mahakama hiyo ya kimataifa kuchukuwa hatua za dharura kukomesha ukiukwaji unaodaiwa kufanywa na Israel.
Rais wa Israel Isaac Herzog aliitaja kesi hiyo ya Afrika Kusini mbele ya mahakama ya ICJ kuwa "ya kikatili na ya kipuuzi". Israel inadai kuwa inafanya juhudi kubwa kuepusha maafa ya raia huko Gaza.
"Tutawasili katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki na tutawasilisha hoja zetu kwa fahari katika kesi hii, tukitumia haki yetu ya msingi ya kujilinda chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu," aliongeza Herzog.
Mahakama ya ICJ itaanza rasmi kusikiliza shauri hilo leo Januari 11 na 12 ambapo Afrika Kusini na Israel zote kwa pamoja zitakuwa na saa mbili katika siku tofauti kutoa utetezi dhidi ya hatua za dharura.
Matokeo ya kesi hiyo
Katika shauri hilo ambalo limevuta nadhari ya kimataifa hakutakuwa na mashahidi wa kutoa ushaidi wao wala wasaa wa kuuliza maswali. Wasilisho hilo litakalowasilishwa na maafisa wa serikali wakiwa pamoja na wanasheria wengine wa kimataifa litakuwa na hoja lukuki za kisheria.
Ombi la hatua za dharura ni hatua ya kwanza katika kesi hiyo ambayo itachukuwa miaka kadhaa kukamilika kwake. Hatua hizo za awali zinazochukuliwa hutambuliwa kama maamuzi ya muda, amri inayotolewa ili kuzuia mzozo kuwa mbaya zaidi wakati mahakama ikiendelea kuangalia, iwapo mlalamikiwa anayo kesi ya kujibu katika shutuma zinazomkabili.
Mahakama haitatoa uamuzi wa mwisho kuhusu madai ya mauaji ya halaiki ya Afrika Kusini hadi kusikilizwa kwa kesi hiyo juu ya uhalali wake, ambayo kuna uwezekano kuchukua miaka kadhaa zaidi.
Usikilizwaji huu unaoanza leo unalenga uwezekano wa kuchukuliwa kwa hatua za dharura. Mara zote mahakimu katika mahakama hiyo huchukua hatua kama hizo ambazo huyaamuru mataifa husika kutojihusisha na matendo yoyote ambayo yanaweza kuzidisha mzozo wa kisheria.
Soma pia: Afrika Kusini yaishtaki Israel ICJ kwa 'mauaji ya kimbari' Gaza
Kwa hatua za muda, mahakama inabidi kuamua katika mtazamo wa kwanza, itakuwa na mamlaka na ikiwa vitendo vinavyolalamikiwa vinaweza kuwa ndani ya mawanda ya Mkataba wa Geneva juu ya Mauaji ya Halaiki. Hatua itakazochukuwa si lazima ziwe zile zilizoombwa na mlalamikaji.
Afrika Kusini imeiomba mahakama kuamuru Israel isitishe operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza, kukomesha vitendo vyovyote vya mauaji ya halaiki au kuchukua hatua zinazofaa kuzuia mauaji ya halaiki na kutoa ripoti za mara kwa mara kwa ICJ kuhusu hatua hizo.
Maamuzi yanatarajiwa kutolewa baada ya majuma kadhaa ya usikilizwaji wa shauri hilo.
Ikumbukwe kwamba maamuzi ya Mahakama hiyo ya Kimataifa ICJ ni ya mwisho na hayana rufaa, lakini mahakama hiyo haina njia ya kulazimisha yatekelezwe.
Hata hivyo, kama uamuzi utatoka dhidi ya Israel, unaweza kuharibu sifa ya kimataifa ya nchi hiyo na kuiweka kuwa mfano wa kisheria.