1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry aupongeza uongozi wa Angola

5 Mei 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameipongeza dhima ya uongozi wa Angola katika juhudi za kutatua mizozo iliyodumu kwa muda mrefu barani Afrika na ameitaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuheshimu katiba.

https://p.dw.com/p/1Btua
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani akiwa katika kituo cha kwanza cha ziara yake Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani akiwa katika kituo cha kwanza cha ziara yake Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.Picha: Reuters

Kerry wakat akiwasili mjini Luanda mji mkuu wa Angola hapo jana katika kituo cha mwisho cha ziara yake barani Afrika amesema Rais Jose Eduardo dos Santos ameonyesha uongozi muhimu na ametaka kuishukuru Angola kwa uongozi mzuri na ushiriki wake katika kutatua mizozo ambayo imeendelea kuwepo kwa muda mrefu mno barani Afrika.

Kerry anatarajiwa kuwa na mazungumzo na rais huyo wa Angola leo hii.Katika ziara yake kuu ya kwanza Afrika akiwa kama waziri wa mambo ya nje, Kerry anaangazia baadhi ya mizozo ilio na ukatili mkubwa kabisa barani humo.

Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani anayeandamana na Kerry katika ziara hii amesema Angola imekuwa ikitimiza dhima nzuri isio ya kawaida katika juhudi za kutatuwa mizozo kadhaa ya kanda hususan katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Dhima ya Dos Santos

Dos Santos hivi karibuni amekuwa mkuu wa Kundi la Mawasiliano la Kimataifa kwa kanda ya Maziwa Makuu barani Afrika.Afisa huyo amesema Dos Santos amekuwa mtendaji mkubwa kwenye dhima hiyo ya uongozi katika kuwakutanisha pamoja viongozi wa kanda kushirikiana kutafuta ufumbuzi kwa mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kuuendeleza mchakato wake.

Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola.
Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola.Picha: picture-alliance/dpa

Mji mkuu wa Luanda mara nyingi umekuwa ukiandaa mazungumzo ya amani yenye lengo la kukomesha mizozo katika kanda ya Maziwa Makuu, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Angola imeipa Jamhuri ya Afrika ya Kati dola milioni 10 kwa ajili ya kuwalipa mishahara wafanyakazi wa serikali na imependekeza kusaidia kusafirisha vikosi ambavyo yumkini vikahitajika kupelekwa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika kipindi cha usoni.

Marekani ni mmojawapo wa washirika wakuu wa biashara wa Angola ambapo kampuni zake kama vile General Electric, kampuni kubwa kabisa ya nishati ya ConocoPhilips na zile za mafuta za Chevron na Exxon zinaendesha shughuli zake mjini Luanda.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani amewasili Luanda akitokea mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Kinshasa na alianza ziara yake wiki iliopita katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.

Congo yatakiwa kuheshimu katiba

Alipokuwapo nchini Congo Kerry ameihimiza nchi hiyo kuheshimu katiba yake ambayo inaweka vikomo kwa muhula wa rais, wakati tetesi zikiongezeka kwamba Rais Joseph Kabila huenda akataka kuwania kipindi cha tatu.

Akina Mama wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakijifunza ushoni.
Akina Mama wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakijifunza ushoni.Picha: Ali Burafi/AFP/Getty Images

Kerry amewaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na Kabila kwamba kiongozi huyo ana fursa ambayo anaifahamu ya kuendelea kuiweka nchi hiyo kwenye mkondo wa demokrasia.

Kerry ameahidi msaada wa dola milioni 30 ambazo kwa kiasi kikubwa zinatarajiwa kutolewa kwa mashirika yasio ya kiserikali kusaidia uchaguzi halikadhalika mipango ya ujenzi mpya katika maeneo ya mbali yalioathirika na mizozo mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Marekani serikali ya nchi hiyo ina haki ya kuzuwiya msaada wa fedha hizo iwapo mchakato wa uchaguzi huo mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2016 hautokuwa wa wazi na wa kuaminika.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/Reuters

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed