1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta ataka mamlaka ya Kongo iheshimiwe

15 Novemba 2022

Mpatanishi maalum wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uhuru Kenyatta, ametaka kuheshimiwa kwa serikali halali ya nchi hiyo, katiba yake, pamoja na mamlaka yake.

https://p.dw.com/p/4JXBd
Kenia | Wahlkampf - Uhuru Kenyatta
Picha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Rais huyo wa zamani wa Kenya alitowa kauli hiyo usiku wa Jumatatu (Novemba 14) mjini Kinshasa wakati wa mkutano na waandishi wa habari alioufanya baada ya kuzungumza na viongozi mbalimbali, akiwemo Rais Felix Tshisekedi, Tume ya Umoja wa Mataifa (MONUSCO) pamoja na wanadiplomasia.

Kenyatta alikuwa nchini Kongo kwa lengo la kukusanya maoni tofauti ya kutafuta amani na usalama katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo linalokumbwa na makundi yanayomiliki silaha.

Mjumbe huyo maalum wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliahidi kuendeleza kazi hiyo na Rais Joao Lourenço wa Angola ili kufikia lengo, lakini akisisitiza kwamba ni lazima iwepo heshima kwa serikali ya Kongo, katiba na mamlaka. 

"Tunayo serikali iliyochaguliwa ambayo uhalali wake lazima tuulinde. Pili, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina katiba ambayo lazima iheshimiwe na hatimaye, kuheshimiwa kwa mamlaka ya eneo la Kongo." Alisema.

Bunge halitaki mazungumzo na M23

Kombibild Felix Tshisekedi und Paul Kagame
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (kushoto) anaishutumu Rwanda ya Rais Paul Kagame kwa kulisaidia kundi la waasi la M23 mashariki mwa nchi yake.

Mbali na Rais Félix Tshisekedi, MONUSCO na wanadiplomasia, Kenyatta alikutana pia wawakilishi wa jumuiya za Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri, pamoja na wawakilishi wa Bunge la kitaifa.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Kitaifa, Christopher Mboso, alikumbusha kwamba Wakongo ni watu wa amani, lakini alikataa kabisa mazungumzo na kundi la waasi la M23, akisisitiza kwamba "hakuwezi kuwa na majadiliano na magaidi."

"Watu wa Kongo wanataka kuishi kwa amani, kwa udugu na mataifa yote. Kwa hiyo tunatarajia amani, lakini M23 ni kundi la kigaidi na hatujadiliani na magaidi. Ikiwa ni lazima kujadiliana na magaidi, lazima kwanza waweke silaha zao chini na kuondoka maeneo yanayovamiwa kinyume na sheria." Alisema spika huyo baada ya kukutana na Rais Kenyatta.

Kenyata aliwasili Kinshasa siku ya Jumapili, wakati mapigano yakiendelea mkoani Kivu Kaskazini baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 na huku pakiandaliwa mazungumzo yanayopangwa kufanyika tarehe 21 Novemba jijini Nairobi, Kenya.  

Imeandikwa na Jean Noel Ba-Mweze/DW Kinshasa