Kenyatta ataka jeshi la Afrika Mashariki litumwe DRC
16 Juni 2022Katika taarifa yake, Rais Kenyatta hapo Jumatano alisema Jeshi la Kikanda la Afrika Mashariki litatumwa katika mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mara moja ili kuleta utulivu katika maeneo hayo na kulisaidia jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika juhudi zake za kuleta amani kwa ushirikiano wa karibu na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO.
Wito huu wa Kenyatta unakuja wakati ambapo kundi la waasi la M23 linafanya mashambulizi makali mashariki mwa Kongo. Waasi hao hapo Jumatatu walitangaza kwamba wameuteka mji wa kimkakati ulioko katika mpaka wa Uganda wa Bunagana.
Haibainiki iwapo Rwanda nayo itajumuishwa kwenye kikosi
Nchi saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambayo Kongo ilijiunga mwaka huu, zilikubaliana mwezi Aprili kuunda kikosi cha pamoja cha jeshi ila hazikubainisha ni lini kikosi hicho kitakapotumwa.
Lakini sasa Kenyatta anasema wakuu wa jeshi wa kanda ya Afrika Mashariki watakutana Jumapili mjini Nairobi ili kumalizia maandalizi ya kutumwa kwa kikosi hicho cha pamoja.
Hakujatolewa tangazo hasa la nchi zitakazojumuishwa kwenye kikosi hicho cha kijeshi cha kanda ya Afrika Mashariki na haijabainika wazi iwapo Rwanda nayo itakuwa miongoni mwa nchi zitakazowasilisha wanajeshi wake.
Taarifa ya Rais Kenyatta pia haikuweka wazi iwapo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imeidhinisha kutumwa kwa kikosi hicho. Maafisa kutoka serikali ya Kongo hawakuweza kupatikana ili kutoa tamko kuhusiana na suala hilo baada ya taarifa ya rais huyo wa Kenya kutolewa.
Rwanda inaendelea kukanusha kuwaunga mkono M23
Wiki kadhaa za mapigano zimepelekea kuibuka kwa mzozo wa kidiplomasia kati ya Kongo na jirani yake Rwanda huku Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ikimlaumu huyo jirani yake kwa kwa kuibuka tena kwa waasi wa M23.
Rwanda mara kadha imekanusha kuwaunga mkono waasi hao na nchi zote mbili zimetuhumiana kwa kufanya mashambulizi ya mabomu katika mipaka ya nchi zao.
Rwanda na Uganda ziliivamia Kongo mara mbili katika miaka ya 1990 uvamizi uliosababisha vita vilivyopelekea vifo vya mamilioni ya watu na kuzuka kwa makundi ya wanamgambo ambayo mpaka wa leo yanaendelea na shughuli zake.
Chanzo: Reuters/AFP