Katibu Mkuu UN Guterres kushiriki Mkutano wa BRICS Urusi
23 Oktoba 2024Mkutano huu ni jukwaa kubwa la kidiplomasia tangu Urusi kuivamia Ukraine mwaka 2022, ambapo Rais Putin anataka kuonyesha kuwa juhudi za kuitenga Urusi kimataifa zimegonga mwamba.
Viongozi takriban 20, wakiwemo wa China, India, Uturuki, na Iran, wanakutana Kazan kujadili mfumo wa malipo wa kimataifa unaoongozwa na BRICS na mzozo wa Mashariki ya Kati.
Moscow inaliona jukwaa hili kama mbadala wa mashirika ya kimataifa yanayoongozwa na Magharibi kama G7, msimamo unaoungwa mkono na Rais wa China, Xi Jinping.
Matokeo ya mazungumzo ya pande mbili
Katika mazungumzo ya pande mbili Jumanne, pamoja na Xi na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, Putin alisifu uhusiano wa karibu wa Moscow na "ushirikiano wa kimkakati" na washirika wake.
Xi alisifu uhusiano wa kina wa China na Urusi, akisema umeleta msukumo mkubwa katika maendeleo na uboreshaji wa nchi hizo mbili katika ulimwengu huu wenye vurugu.
Putin alisema anauona uhusiano kati ya Beijing na Urusi kama msingi wa "utulivu" wa kimataifa. "Ushirikiano wa Kirusi na Kichina katika masuala ya dunia ni moja ya sababu za kuleta utulivu katika uwanja wa kimataifa.
Tunakusudia kuongeza uratibu zaidi katika majukwaa yote ya kimataifa ili kuhakikisha usalama wa dunia na utawala wa haki," alimuambia Xi.
Viongozi hao watafanya kikao leo Jumatano ambapo wanatarajiwa kusisitiza jukumu la BRICS katika kuimarisha kile ambacho Moscow na Beijing zinakitaja kama "mpangilio wa ulimwengu wa pande nyingi."
Putin atafanya mazungumzo ya pande mbili na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian na Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, pamoja na kukutana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye anajitahidi kujihusisha kama mpatanishi kati ya Urusi na Ukraine huku akiendeleza uhusiano mzuri na Moscow licha ya kuwa mwanachama wa NATO.
Kyiv yakomkosa Guterres kwa kuitikia mwaliko wa "mhalifu wa kivita"
Guterres atakutana na Putin Alhamisi kujadili mzozo wa Ukraine, kulingana na Kremlin. Kyiv imekosoa ziara hiyo, ikisema Guterres alikataa mwaliko wa Mkutano wa Amani wa Uswisi lakini alikubali mwaliko wa Kazan kutoka kwa Putin, inayemuita "mhalifu wa kivita."
Msemaji wa Guterres amesema ziara hiyo ni sehemu ya ushiriki wake wa kawaida kwenye mashirika muhimu na inampa nafasi ya kuimarisha misimamo yake kuhusu mzozo wa Ukraine na masharti ya amani ya haki.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, akijitambulisha kama mpatanishi, alitoa wito wa kumalizwa haraka kwa mzozo wakati wa mazungumzo na Putin Jumanne, akisisitiza kuwa India inaamini mizozo inapaswa kutatuliwa kwa amani.
India imekuwa ikiunga mkono Kyiv kibinadamu bila kulaani wazi hatua za Moscow, huku Urusi ikiendelea kusonga mbele mashariki mwa Ukraine na kuimarisha uhusiano na China, Iran, na Korea Kaskazini.
Soma zaidi: Mkutano wa BRICS: Putin akutana na viongozi mbalimbali
Rais Putin amewaambia wajumbe wa mkutano wa BRICS Jumatano kwamba zaidi ya nchi 30 zimeonyesha nia ya kujiunga na kundi hilo.
Putin amesema kundi hilo litajadili upanuzi wake katika mkutano huo, huku wakizingatia umuhimu wa kudumisha ufanisi.