Katiba ya Tanzania inasemaje baada ya kifo cha Rais?
18 Machi 2021Mjadala wa vipi makamu wa rais wa Tanzania anapaswa kuapishwa kuwa rais wa taifa hilo, umeanza kushika kasi licha kwamba Katiba nchini humo kueleza bayana hatua zinazopaswa kufuatwa iwapo rais aliyeko madarakani ataachia madaraka kwa sababu mbalimbali ikiwemo kifo.
Katiba inasema kuwa, Rais aachiapo madaraka kwa sababu ya aina yoyote ile, makamu wake ataapishwa kuchukua nafasi hiyo na mara baada ya kufanya hivyo atajadiliana na chama chake cha siasa kwa ajili ya kumteua makamu wa rais.
Na wakati huu ambapo taifa likiendelea na maombolezo ya kifo cha Rais John Magufuli aliyeaga dunia Jumatano jioni, kinashosubiriwa sasa ni kwa namna gani makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan atakula kiapo cha kuwa Rais Mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mara ya kwanza Tanzania yaondokewa na kiongozi wa nchi akiwa bado madarakani
Kwa vyovyote vile, Tanzania itakuwa imeingia katika rekodi mpya ya kuondokewa na kiongozi wa nchi akiwa bado madarakani na itaandika historia mpya kwa kuwa na Rais wa kwanza mwanamke tangu ilipoanza kujitawala mwaka 1961.
Ingawa wengi wanaojadili suala hili na makamu wa rais kuchukua nafasi ya urais kamili wanafanya hivyo kwa kuzingatia mwongozi wa kikatiba, hata hivyo baadhi yao wanajikuta wakiingia kwenye mtego wa kushindwa kufafanua bayana hatua zinazopaswa kufuata.
Baadhi ya wataalamu wa sheria wanasema katiba imetoa mwongozo unaoleweka inapotokea tukio kama hili lakuondokewana kiongozi wake mkuu.
Mwanahabari wa siku nyingi na msomi wa sheria, Deudatus Balile anasema katiba ya nchi imeweka bayana muda ambao makamu wa Rais anapaswa kupishwa kuwa Rais kamili tangu Rais aliyekuwa madarakani kuachia wadhifa wake huo.
Tanzania kwa sasa iko katika maombolezo ya siku 14, huku wananchi wake wakiendelea kusubiri kujua jinsi taratibu za mazishi ya mpendwa wao, Rais John Magufuli aliyeaga dunia akiwa amekaa madarakani kwa miaka sita.
Rais Magufuli alionekana hadharani kwa mara ya mwisho ilikuwa Februari 27 wakati alipokuwa akimwapisha Katibu Mkuu Kiongozi mpya, Dr Ally Bashiru kufuatia kufariki dunia kwa katibu mkuu kiongozi wa awali John Kijazi ambaye aliga dunia Februari 17.
Lakini kabla ya hapo, Rais Magufuli alionekana hadharani mara kadhaa ikiwamo katika matukio ya uzinduzi wa daraja jipya la juu eneo la Ubungo na kituo cha mabasi ya kimataifa eneo la Mbezi Luisi.
Na salamu za rambirambi zinaendelea kumimini kutoka kona mbalimbali, nyingi zikielezea utendaji kazi wa kiongozi huyo aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 61.