1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karani wa kambi ya Kinazi apandishwa kizimbani

19 Oktoba 2021

Karani wa zamani wa kambi ya mateso ya Kinazi mwenye umri wa miaka 96 ambaye aliwahi kukimbia kabla ya kuanza kwa kesi yake, hatimaye amepandishwa kizimbani leo Jumanne akikabiliwa na mashtaka ya kuhusika na mauaji.

https://p.dw.com/p/41rsR
Deutschland | Prozess gegen ehemalige KZ-Sekretärin in Itzehoe
Picha: Markus Schreiber/AFP/Getty Images

Bibi huyo Irmgard Furchner, ambaye ni mwanamke wa kwanza kushtakiwa kwa makosa yaliyofanyika wakati wa utawala wa Kinazi, anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya zaidi ya watu 11,000 katika kambi ya Stutthof iliyokuwa inakaliwa kimabavu nchini Poland.

Mkongwe huyo alifikishwa katika mahakama ya mkoa iliyoko katika mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Itzehoe akiwa ameketi kwenye kiti cha marugudumu, huku akifunika kichwa chake kwa skafu pamoja na kuvaa barakoa.

Lilikuwa ni jaribio la pili kwa kesi dhidi ya bi. Furchner kusikilizwa baada ya kuikimbia nyumba ya wazee alimokuwa akiishi mnamo Septemba 30, wakati kesi yake ilipokuwa inaanza.

Soma pia: Mlinzi wa miaka 100 wa enzi ya Manazi kushitakiwa kwa mauaji

Mshtakiwa huyo alifanikiwa kuikwepa mitego ya polisi kwa saa kadhaa kabla ya hatimaye kukamatwa katika mji wa karibu wa Hamburg.

Msemaji wa mahakama Frederike Milhoffer amesema bibi huyo aliachiliwa siku tano baadaye, chini ya tahadhari kali. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, mshtakiwa huyo aliwekewa vifaa maalum vya kielektroniki ili kufuatilia mienendo yake.

Kati ya Juni mwaka 1943 na Aprili 1945, mshtakiwa huyo alikuwa akifanya kazi kama karani katika ofisi ya kamanda Paul Werner Hoppe. Waendesha mashtaka wanasema alikuwa akichukua maagizo ya walinzi wa utawala wa kinazi wa SS na kushughulikia barua zao.

Walinzi wa utawala wa kinazi SS walianzisha kambi za mateso waliowaua watu kikatili

Gedenkstätte Konzentrationslager Stutthof
Kambi ya mateso ya Stutthof iliyozuia wafungwa wa KiyahudiPicha: Getty Images/B. Adams

Kwa mujibu wa mashtaka yaliyosomwa kortini, watu wapatao 65,000 walikufa katika kambi ya Stutthof karibu na mji wa Gdansk, miongoni mwao wafungwa wa Kiyahudi, washirika wa Poland na wafungwa wa iliyokuwa Umoja wa Kisovieti.

Mwendesha mashtaka amesema kazi ya ukarani ya bi. Furchner ilihakikisha uendeshaji mzuri wa kambi hiyo ya mateso na kwamba alifahamu vyema matukio yote ya kinyama yaliyokuwa yakifanyika katika kambi ya Stutthof ikiwemo mauaji ya halaiki.

Mwendesha mashtaka ameendelea kusema kuwa, mateso ya wahanga pamoja na vilio vya watu waliopelekwa kwenye vyumba vya gesi ya sumu vilisikika na kila mtu aliyekuwa katika kambi hiyo.

Soma pia: Miaka 70 ya kukombolewa kwa kambi ya mateso Buchenwald

Katika barua iliyotumwa kabla ya kuanza kwa kesi hiyo, mshtakiwa alimuelezea jaji kwamba hangependelea kufika kizimbani binafsi.

Makamu wa rais wa kamati iliyoanzishwa na manusura wa kambi ya mateso ya Auschwitz Christoph Heubner, aliliambia shirika la habari la AFP wakati huo kuwa, kukosa kwake kufika mahakamani mnamo mwezi Septemba kulionyesha dharau kwa wahanga na pia kuidharau sheria.

Efraim Zuroff, mwindaji wa walinzi wa kinazi aliyekuwa na jukumu muhimu katika kuwafikisha mahakamani wahalifu katika utawala wa kinazi ameandika katika mtandao wake wa Twitter, "Kama ana afya ya kutosha ya kukimbia mkono wa sheria, basi pia ana afya ya kwenda jela."

Miaka 76 imepita baada ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya dunia, muda unayoyoma kwa wahalifu waliohusika na mauaji katika kambi za mateso kuwajibishwa.