1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani Scholz kukutana na Biden Washington

Josephat Charo
7 Februari 2022

Huku mawingu ya vita yakitanda katika anga la Ukraine juhudi za kidiplomasia zinashika kasi Jumatatu (07.02.2022) huku kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akitarajiwa kukutana na rais wa Marekani Joe Biden mjini Washington.

https://p.dw.com/p/46cDq
Bundeskanzler Olaf Scholz
Picha: Michael Kappeler/AP/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesafiri kwenda Washington kuwahakikisha Wamarekani kwamba nchi yake inaiunga mkono Marekani na washirika wengine wa jumuiya ya kujihami ya NATO katika kupinga aina yoyote ya uchokozi wa Urusi dhidi ya Ukraine. Scholz amesema Urusi italipa gharama kubwa iwapo ifafanya shambulizi, lakini hatua ya serikali yake kukataa kupeleka silaha hatari za maangamizi nchini Ukraine, kuongeza idadi ya wanajeshi Ulaya Mashariki au kutaja vikwazo itakavyoviunga mkono dhidi ya Urusi, imeibua ukosoaji ndani na nje ya Ujerumani.

Akizungumza na waandishi habari kabla kuondoka mjini Berlin, Scholz amesisitiza Ujerumani inatimiza wajibu wake. "Katika Umoja wa Ulaya, barani Ulaya sisi ni nchi yenye mchango mkubwa wa ulinzi. Tuna wanajeshi nchini Lithuania. Tunahakikisha usimamizi wa anga katika mpaka wa NATO unafanyika barabara, na wakati huo huo sisi ndio tumekuwa tukitoa msaada mkubwa wa kifedha kwa Ukraine kwa miaka mingi. Ndio wafadhaili wakubwa tangu mwaka 2014 kwa msaada wa kiuchumi na kifedha."

Ukosoaji pia umejikita juu ya utegemezi mkubwa wa Ujeruamni kwa gesi asili kutoka kwa Urusi na ujenzi wa bomba la gesi la Nord Stream 2 litakalotumiwa kusafirisha gesi hadi Ujerumani kupitia chini ya bahari ya Baltic, na kuikwepa Ukraine. Mradi huo umepingwa na Marekani lakini unaungwa mkono sana na chama cha Scholz cha Social Democratic, SPD, hasa kansela wake wa zamani, Gerhard Schroeder.

Katika hatua ambayo huenda ikamtia aibu na kumuweka katika kiti moto kansela Scholz katika zaira yake ya kwanza Washington, kampuni ya gesi inayomilikiwa na serikali ya Urusi, Gazprom, siku ya Ijumaa ilitangaza kwamba Schroeder, ambaye ameituhumu Ukraine kwa kutoa kauli na kufanya vitendo vinavyochochea hatua ya kijeshi dhidi yake, ameteuliwa kujiunga na bodi ya wakurugenzi ya kampuni hiyo.

Scholz anatarajiwa kukutana na rais Biden na wabunge la Marekani, huku mkutano na waandishi habari na mahojiano maalaumu yakiwa pia katika ratiba ya ziara yake. 

USA | Präsident Joe Biden | zum Schlag gegen den IS
Joe Biden, rais wa MarekaniPicha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Biden ametoa vikosi 3,000 vya wanajeshi wa Marekani kuimarisha eneo la mashariki la jumuiya ya kujihami ya NATO, huku kundi la kwanza la wanajeshi hao wakiwasili nchini Poland jana Jumapili. Hata hivyo mshauri wa kitaifa wa masuala ya usalama wa Marekani, Jake Sullivan, ameiambia Fox News siku ya Jumapili kwamba Biden hapeleki wanajeshi kuanzisha vita au kupigana na Urusi nchini Ukraine, bali kuilinda Ukraine. Sullivan ameonya kwamba Urusi huenda ikaivamia Ukraine siku yoyote na kuanzisha mzozo ambao yumkini ukasababisha gharama kubwa ya kibinadamu.

Baada ya ziara yake ya Marekani, kansela Scholz anatarajiwa kwenda Urusi na Ukraine wiki ijayo kwa mazungumzo na rais Putin na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambaye nchi yake inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, atakuwa mjini Moscow Jumatatu na kusafiri hadi mjini Kyiv siku ya Jumanne kuongoza juhudi za kidiplomasia kujaribu kutuliza hali ya wasiwasi na kuutafutia ufumbuzi mgogoro unaeoendelea kufukuta. Anatarajiwa kuendeleza mpango wa amani uliokwama na waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine. Ziara hiyo itakuwa kama kamari ya kisiasa kwa Macron ambaye anakabiliwa na changamoto katika uchaguzi wa mwezi Aprili nchini mwake.

Taarifa ya ikulu ya Marekani mjini Washington imesema Macron alizungumza kwa njia ya simu na rais Biden Jumapili kabla kuelekea Moscow, ambapo walizungumzia juu ya juhudi za kidiplomasia zinazoendelea kujaribu kuepusha uvamizi wa Urusi na kusisitiza msimamo wao wa kuunga mkono uhuru wa Ukraine na heshima ya mipaka yake. Macron pia alizungumza na kansela Scholz kuhusu msimamo wake kabla kwenda Moscow.

Jumatatu pia mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Jamhuri ya Czech, Slovakia na Austria wanatarajiwa kukutana mjini Kyiv nchini Ukraine, ambayo imepuuza onyo kali la Marekani kwamba Urusi imeongeza juhudi za maandalizi ya kufanya uvamizi mkubwa nchini humo. Maafisa wa Marekani wamesema Urusi imetuma vikosi 110,000 vya wanajeshi katika mpaka na Ukraine lakini tathmini ya kijasusi haijabaini ikiwa rais Vladimir Putin ameamua kweli kuvamia. Maafisa hao aidha wamesema Urusi iko njiani kuwapeleka wanajeshi kiasi 150,000 kwa uvamizi kamili kufikia katikati ya mwezi huu wa Februari.

afp, dpa, ap