Ujerumani hatopeleka makombora ya masafa marefu Ukraine
15 Septemba 2024Ameendelea kuushikilia msimamo huo alipokuwa akifanya mazungumzo na wananchi katika mji wa Prenzlau jimboni Brandenburg. Scholz ameeleza kuwa kuyapeleka Ukraine makombora ya Taurus yenye uwezo wa kusafiri umbali wa kilometa 500 kutazidi kuhatarisha hali katika mzozo huo.
Soma zaidi: Ukraine yaihimiza Ujerumani kuipatia makombora ya Taurus
Mataifa washirika yaliyo chini ya Jumuiya ya kujihami ya NATO, ambayo ni Marekani, Uingereza na Ufaransa, yamekubali kuipatia Ukraine makombora yenye uwezo wa kusafiri umbali wa kilometa 300 licha ya kuendelea kwa mjadala ikiwa makombora hayo yaidhinishwe kutumiwa dhidi ya maeneo ya Urusi ama la.
Soma zaidi: Bunge la Ujerumani lakataa kuitumia Ukraine makombora ya masafa marefu
Rais Vladmir Putin wa Urusi ameshasema kuwa atayatizama matumizi ya makombora ya masafa marefu ndani ya ardhi yake kuwa ni uhusika wa moja kwa moja wa Jumuiya ya kujihami ya NATO katika vita hivyo.