Kansela Merkel autetea msimamo wake kuhusu wakimbizi bungeni
28 Juni 2018Kansela Markel amesisitiza kuwepo suluhisho la pamoja la Umoja wa Ulaya na amesema umoja huo bado haujaweza kupata suluhisho la pamoja juu ya suala la wakimbizi. Amewaambia wabunge wa Ujerumani leo kwamba viongozi wa Umoja wa Ulaya hawajafika wanakolenga kufikia.
Hotuba yake ilikatizwa mara kwa mara na wabunge wa chama cha mrengo mkali wa kulia maarufu kama chama mbadala (AfD). Kiongozi huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa vipengele viwili kati ya saba juu ya mpango unotayarishwa kwa pamoja na washirika wengine wa Umoja wa Ulaya bado ni wa utatanishi na kwamba unapaswa kutatuliwa mnamo siku mbili zijazo. Amesema kipengele kimojawapo kinahusu agizo la Umoja wa Ulaya juu ya haki za kimataifa, ambapo nchi wanachama zinapaswa kuwa na vigezo vya pamoja juu ya kutoa hifadhi kwa wakimbizi.
Bibi Merkel pia amezungmzia juu ya kipengee kinachohusu mkataba wa Dublin unaofafanua juu ya nchi ambako wakimbizi wanatoa maombi na jinsi nchi zinavyoweza kugawana jukumu la kuwachukua wakimbizi hao. Amesema masuala hayo bado yana utatanishi miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya.
Ikiwa Kansela Merkel atashindwa kupata suluhisho la pamoja la Umoja wa Ulaya juu ya namna ya kugawana jukumu la wakimbizi na namna ya kuyashughulikia maombi ya wakimbizi hao, shinikizo linalomkabili hasa kutoka kwa washirika wake wa chama ndugu cha CSU litazidi kuwa gumu kulihimili. Hata hivyo kiongozi huyo wa Ujerumani amesisitiza kwamba suluhisho la mgogoro wa wakimbizi litaweza kupatikana kwa kufanya mazungumzo na serikali za nchi za Afrika sawa na jinsi mazungumzo yalivyofanyika na kufikia suluhisho na Uturuki.
Wabunge wa chama cha mrengo wa shoto wamekilaumu chama cha CSU kwa kulitumia suala la wakimbizi ili kujinufaisha kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika katika jimbo la Bavaria la kusini mwa Ujerumani ambalo ni maskani makuu ya chama hicho. Chama cha Christian Social Union (CSU) kinataka wakimbizi waliosajiliwa wazuiliwe mpakani. Mbunge wa chama cha mrengo wa shoto Sarah Wagenknecht amesema sera hiyo itasababisha mvutano mwingine katika uhusiano baina ya nchi za Umoja wa Ulaya.
Akichangia kwenye mjadala wa bunge leo kiongozzi wa chama cha Waliberali (FDP) Christian Lindner ameelezea mashaka yake iwapo viongozi wa Umoja wa Ulaya watafikia suluhisho la mgogoro wa wakimbizi kwenye mkutano wao wa siku mbili unaoanza leo mjini Brussels.
Hata hivyo bwana Lindner amesema mgogoro wa wakimbizi haupaswi kuwa suala pekee katika ajenda za siasa nchini Ujerumani. Amesema msimamo wa chama cha CSU wa kuushikilia mgogoro huo umemweka Kansela wa Ujerumani katika hali ngumu na kumfanya aweze kushinikizwa kwenye Umoja wa Ulaya. Naye mwenyekiti wa chama cha Social Demokratic SPD Andresa Nahles amevitaka vyama vya CDU na CSU vimalize mvutano wao juu ya suala la wakimbizi na kurejea katika masuala mengine muhimu.
Mwandishi: Zainab Aziz/RTRD/p.dw.com/p/30S5e
Mhariri: Iddi Ssessanga